.

Mambo 20 Ya Kujifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha How To Stop Worrying And Start Living

Na: MAKIRITA Amani.

MAMBO 20 NILIYOJIFUNZA KWENYE KITABU HOW TO STOP WORRYING AND START LIVING.
Kitabu HOW TO STOP WORRYING AND START LIVING ni kitabu ambacho kimeeleza mbinu bora sana za kuondokana na hofu na mashaka kwenye maisha. Maisha yaliyojawa hofu ni maisha mabovu sana na ni vigumu kuweza kufikia mafanikio.

Yafuatayo ni mambo 20 kati ya mengi niliyojifunza kwneye kitabu hiki;
1. Sisi wote tunajua vitu vingi sana vya kututosha kuwa na maisha bora. Tatizo letu sio ujinga au kutokujua nini cha kufanya, bali tatizo letu ni kutokuwa tayari kuchukua hatua. Hata uwe unajua vitu vingi kiasi gani, bila ya kuchukua hatua ni kazi bure. Unahitaji ujasiri wa kuwez akufanyia akzi vile unavyojifunza ndio maisha yako yaweze kuwa bora.

2. Jukumu letu kubwa kwenye maisha sio kuona na kuhofia yale yatakayotokea mbele, bali kufanyia kazi yale ambayo yapo kwenye mikono yetu sasa. Njia bora kabisa ya kuondokana na hofu ni kuishi leo. Jana imeshapita na huwezi kuibadili, kesho haijafika na hivyo hata uhofu vipi huwezi kubadili chochote. Ila leo, muda huu upo mbele yako na unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya.

Ishi leo, weka mawazo yako yote kwneye hiko unachofanya leo na sehemu kubw aya hofu itatoweka.

3. Kama bado unaihofia kesho yako jua kitu hiki muhimu sana, njia bora kabisa ya kuwa na kesho bora ni kuishi vizuri leo. Kama unataka kuwa na kesho bora na yenye mafanikio, kama unataka kehso yako isiwe ya hatari, basi ishi vizuri sana leo. Fanya kile ambacho ulipanga kufanya leo na kifanye kw aubora. na kesho itakapofika utakuwa na sehemu nzuri ya kuanzia. Ila kama utapoteza muda wa leo kuhofu kuhusu kesho, kesho itafika ukiw ahujajiandaa kwa lolote na hivyo hofu yako itakuwa maradufu.

4.  Iwe ni wakati wa vita au amani kuna aina mbili za fira. Aina ya kwanza ni fikra nzuri hizi ni fikra ambazo zinaangalia ni nini chanzo cha tatizo au kitu na kuja na mpango mzuri wa kuchukua hatua. Aina ya pili ni fikra mbaya, hizi ni zile fikra ambazo zinaleta msongo wa mawazo na hata ugonjwa wa akili(kuchanganyikiwa)

5. Hata uwe na mambo mengi vipi ya kufanya kwa siku, bado huwezi kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Unaweza kufanya kitu kimoja vizuri kwa wakati mmoja. Sasa chanzo cha wengi kuwa na hofu ni pale wanapojaribu kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja, kulazimisha kufanya vitu ambavyo hawawezi kufanya kwa wakati huo. Panga siku yako na fanya kitu kimoja wka wakati, utaondokana na hofu nyingi.

6. Kitu kingine ambacho kinajenga maisha ya hofu na mashaka ni tabia ya watu wengi ya kuahirisha maisha. Huwa tunajidanganya kwamba siku zijazo tutakuwa na maisha bora sana. Mtoto anasema nikimaliza kusoma maisha yangu yatakuwa bora, akimaliza kusoma anasema nikipata kazi maisha yangu yatakuwa mazuri, akipata kazi anasema nikiwa na familia maisha yangu yatakuwa mazuri, akipata familia anasema watoto wakishakuwa maisha yatakuwa mazuri. watoto wakishakua anasema nikistaafu maisha yangu yatakuwa mazuri. Akistaafu anajikuta muda umeenda na kujiuliza alikuwa wapi hakuishi.
Sikiliza, maisha yako ni sasa, kama unataka kuwa na maisha bora, unaanzakuwa nayo leo na sio kesho, hiyo kesho unayosubiri haitafika.

7. Unapokuwa na wasiwasi huwezi kufanya jambo lolote zuri kwenye shughuli zako wala maisha yako. Hii ni kwa sababu wasiwasi hutawala akili yako na hivyo kushindwa kufikiri sawasawa na kuituliza akili yako ili iweze kufanya maamuzi sahihi. Hata kama tatizo ni dogo kiasi gani, ukishakuwa na wasiwasi mkubwa unashindw akulitatua. Ni muhimu sana kuondokana na wasiwasi kwanza ili kuwez akufanya maamuzi sahihi.

8. Kubali hali mbaya inayoweza kutokea. Mara nyingi wasiwasi hutokana na kutokuwa na uhakika wa nini kitatokea. Hivyo unashindw akufanya maamuzi kwa sababu huna uhakika wa kitakachotokea mbeleni. Ili kuondokana na hili, kubaliana na hali mbaya kabisa inayoweza kutokea. Fikiria ni kitu gani kibaya sana kinachoweza kutokea kama utachukua hatua. Kubaliana nacho halafu chukua hatua, mara nyingi kile ulichokuwa unafikiri kitatokea wala hakitatokea na maisha yako yatakuwa bora sana.

9. Watu wengi wanaokwenda mahospitalini hawana ugonjwa wowote mkubwa, bali wamejawa na wasiwasi mkubwa na hivyo wasiwasi huu unaanza kudhoofisha mwili. Watu wanapata vidonda vya tumbo, maumivu ya mwili, kukosa usingizi, kuumwa kichwa, yote hayo sio kwa sababu kuna tatizo kwenye miili yao, ila akili zao zimezidiwa na hofu na hivyo kuufanya mwili kuwa dhaifu au kutengeneza ugonjwa ambao utampa mtu sababu ya kukimbia tatizo ambalo linamkabili.

10. Ni kitu gani kinasababisha ugonjwa wa akili(kuchanganyikiwa)? Kuna vitu vingi vinasababisha, ila kimoja wapo ni hofu na wasiwasi uliopitiliza. Mtu ambaye ana wasiwasi sana na anayeshindw akukabiliana na changamoto za dunia huishia kutoroka changamoto hizi kwa kujitengenezea dunia yake mwenyewe. Hivyo anaongea na watu anaowaona yeye mwenyewe, nyie wengine hamuwaoni, anasikia sauti yeye mwenyewe wengine hawasikii. Kuepuka kufika huku, anza kufanyia kazi tatizo lako la hofu na wasiwasi.

11. Kama unayapenda maisha na kama unapenda kuwa na maisha bora, basi unahitaji kuweza kutuliza akili yako na mawazo yako bila ya kujali ni nini kinaendelea kwenye maisha yako. Ukiwa mtu wa kutaharuki na kuwa na wasiwasi mkubwa, kwa dunia ya sasa ambayo imejaa kila changamoto kila wakati utaona maisha yako ni mabovu sana. Chochote kinachotokea tuliza akili yako na jiulize ni kitu gani kibaya zaidi kinaweza kutokea na hatua gani unaweza kuchukua

12. Kama mtu atakuwa na ujasiri wa kuziendea ndoto zake, bila ya kujali ni nini kinaendelea kwenye maisha yake, ni lazima atakutana na mafanikio katika kile anachofanya. Unachohitaji ni ujasiri wa kuweza kuendelea licha ya changamoto unazipitia, Na utapata ujasiri huu kama utaweza kutuliza wasiwasi mkubwa unaokuwa nao katika nyakati ngumu.

13. NJIA YA UHAKIKA YA KUONDOKANA NA HOFU NA WASIWASI.

Kuna hatua nne muhimu unazoweza kutumia na ukashinda hofu au wasiwasi wowote unaokutawala kwenye maisha yako.
1. Jua wasiwasi huo unatokana na nini na jua kila kitu ambacho kinasababisha wasiwasi huo. Jua mengi kuhusiana na wasiwasi huo.
2. Chambua kila sababu ambayo imepelekea wewe kuwa na wasiwasi huo. Pata mawazo mengi zaidi ya jinsi ya kutatua changamoto iliyopelekea kupata wasiwasi huo.
3. Amua ni hatua gani utakayochukua ili kuondokana na hofu hiyo na kutatua tatizo ulilonalo. Jua ni jambio gani baya linalowez akutokea kwa hatua utakayochukua na kubaliana nalo.
4. Chukua hatua mara moja na usirudi tena nyuma kufikiria mara mbili mbili.
14. Nusu ya hofu na wasiwasi mkubwa wanaopata watu duniani unatokana na watu kujaribu kufanya maamuzi bila ya kuwa na taarifa za kutosha.  Watu wengi hikimbilia kufanya maamuzi na kukuta yale maamuzi yanaleta matatizo zaidi. Jipe muda wa kujua tatizo vizuri, fikiria njia zote unazoweza kutumia na chagua njia ambayo unakubaliana na matokeo yake.
15. Binadamu wako radhi wafanye kitu chochote ili mradi tu waepuke kazi ya kufikiri. Watu wengi hujaribu kukwepa matatizo waliyonayo kwa kutokuyafikiria vyema na hii huzidi kuwaletea hofu na wasiwasi. Wengine hutumia vilevi wakiamini vinawaondolea wasiwasi, ila ulevi unapoisha matatizo yanakuwa pale pale. Kuindokana na hofu na wasiwasi, tatua changamoto inayokukabili.
16. Kuendelea kufikiria tatizo kwa muda mrefu bila ya kufikia kwenye suluhisho kunaongeza hofu na wasiwasi. Hivyo jiwekee utaratibu ambapo unapokuwa na tatizo au changamoto yoyote unaipa muda wa kuifanyia kazi na usiende muda zaidi ya huo uliojipangia.
17. Njia nyingine bora yakuondokana na wasiwasi ni kutokuipa akili yako nafasi ya kujawa na wasiwasi. Akili yako ni kama debe, debe likiwa limejaa linatulia, ila likiwa tupu linapiga kelele. Akili yako ikiwa na mambo ya kufanya na kufikiria mawazo ya hofu na wasiwasi hayapati nafasi. Ila akili yako inapokuwa tupu na haina majukumu hapa ndipo mawazo ya hofu na wasiwasi yanapopata nafasi ya kukutawala.
18. Jisahau kwenye kufanya kitu ambacho unakipenda na akili yako yote inakifikiria. Mara nyingi watu wanaopata matatizo kwenye kazi ni wale ambao wanafanya kazi ambazo hawazipendi. Hii ni kwa sababu wakati wanafanya kazi mawazo yao yako sehemu nyingine. Ila wale ambao wanapenda kazi zao, mawazo yao yote huwa kwenye kazi zile na huwa wanafanikiwa sana na matatizo yao ni machache. Penda sana unachofanya, utaondokana na wasiwasi mwingi.
19. Maisha ni mafupi sana, kuwa mdogo. Usipoteze muda wako wa thamani sana kwa kuhangaika na vitu vidogo, maana hivi vinakufanya kuwa mdogo na kushindwa kufurahia maisha yako. Vitu hivi vidogo ni vipi? Kushindana kwa mambo madogo, kulipa visasi, kumnunia mtu, kusema watu vibaya, kuona wivu na mengine kama hayo. Una miaka michache sana hapa duniani, usiipoteze kwa kufanya mambo haya ambayo hakuna atakayeyakumbuka siku chache baada ya wewe kufa. Fanya kitu kitakachoacha alama yako hata utakapoondoka.
20. Kabla hujahofu au kuwa na wasiwasi kuhusu kitu, jiulize je ni mara ngapi kitu hiko kimekuwa kinatokea? Mara nyingi huwa tunahofu vitu ambavyo uwezekano wake wa kutokea ni mdogo. Kwa mfano unaishi mjini halafu una hofu kwamba unaweza kuliwa na simba? Hii haileti maana kabisa, kwa sababu ni watu wangapi walishaliwa na simba kwenye mji ambao unaishi?
Ukifikiria kw akina uwezekano wa kila unachohofia kutokea utagundua kwamba unajipa hofu ya bure kwa sababu uwezekano ni mdogo sana.

Previous
Next Post »