.

“Watu Wangu Wanaangamizwa Kwa Kukosa Maarifa”


Na: Meshack Maganga--Iringa,Go Big or Go Home

“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” ni moja ya mistari maarufu sana katika kitabu kitakatifu Biblia. Ni moja ya sentensi zinazoigusa jamii yetu kwa sasa, hapa Tanzania, Afika na dunia kwa ujumla. Kitabu hiki cha ‘Graduate with PlanB in Mind’ kimekuja wakati muafaka kabisa kwa Taifa letu na dunia kwa ujumla. Hii ni kwa sababu
kimetokea wakati ambao vijana wengi  wa kike na wa kiume waliopo katika ngazi mbalimbali za kielimu wamekuwa wakiyumba yumba sana na wasijue cha kufanya wanapokuwa wamehitimu masomo yao. Wengi wao wamekuwa ni wahitimu walalamishi badala ya kuwa wahitimu wafumbuzi wa matatizo ya kijamii inayowazunguka.

Nilipokisoma kitabu hiki kilipokuwa katika hatua za awali, mawazo yangu ya kina yalilipuka upya. Nilitamani kama ningekisoma kitabu hiki mwanzo kabisa nikiwa shule ya sekondari ya kawaida. Nilishasoma vitabu vingi sana vilivyoandikwa kwa Lugha ya Kiswahili, na kingereza vikiongelea namna ya kufanikiwa katika maisha, namna ya kushinda kwenye usaili, na vingine vingi vya aina hiyo. Lakini sikuwahi kusoma kitabu ambacho kingenipatia mbadala wa maisha. (Plan B). 

Wengi wetu tunapotoka vyuo vikuu tunakuwa tumebeba wazo moja kuu la ‘ajira’, kana kwamba ajira ni moja ya amri kumi takatifu za nabii Musa ambazo ukiikosea moja tu unapigwa mawe.  Tunapofika mitaani kwetu tunakuta kitu kingine. Tunapokuwa chuo kikuu ama katika ngazi za chini za elimu tunajisahau sana. Tunakuwa kwenye ulimwengu wa chuo kikuu kana kwamba hatutaondoka kwenye majengo ya vyuo na kutufanya tusahau ulimwengu wa halisi wa mtaani kwetu. 

Kama wewe ni mwanafunzi wa ngazi yoyote ile unayoifahamu, hakikisha unakisoma kitabu  hiki, kwanini uendelee kuangamizwa  kwa kukosa maarifa na kuendelea kuamini  mawazo ya walioshindwa ama kubebwa na matukio ya mitaani ama kwenye mitandao ya kijamii? Ama mawazo ya wanafunzi wenzako na mawazo ya walimu na wazazi waoishi maisha ya uoga? Wanaoamini kwamba maisha ni ajira pekee?  Tumekuwa watu wenye kubebwa na wazo moja tu la ajira kana kwamba bila ajira maisha hayaendi. 

Tumechelewa sana kuangalia na kujifunza kwa wenzetu wa nchi za dunia ya kwanza ambako maisha ni zaidi ya ajira. Tupo kwenye dunia ambayo wasomi na wajasiriamali wanatakiwa kuwa wabunifu wabuni ajira,maana kila anaehitimu akiwaza kuajiliwa basi kuna hatari ya kuwa wategemezi kwenye vipengele mbalimbali vya maisha. Bahati nzuri Tanzania ni moja ya nchi pekee duniani iliyosheheni fursa za kila aina fursa unazoweza kuzifanya hata kabla ya kutoka shule ama chuo. Uamuzi unabakia mkononi mwako, kujifunza maarifa na kuzitumia fursa ama kutojifunza ili ukihitimu masomo yako ubakie kuwa mlalamikaji.

Mawazo yaliyo andikwa na Mwandishi wa kitabu hiki ni mawazo yaliyofanyiwa utafiti wa kina na lengo lake ni kuzalisha mitazamo mipya miongoni wa wasomi waliopo vyuoni, wazazi, walimu, viongozi mbalimbali wa kisiasa, kidini na kijamii kwa ujumla. Ninatoa rai yangu kwa wazazi, walimu na wakuu wa vyuo na shule kukinunua kitabu hiki na kukiweka kwenye maktaba zao ili kiwe msaada kwa wanafunzi na watoto wao.

 Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani wanaweza.Siyo dunia ya kufuata mkumbo wala bendera kufuata upepo na matukio ya kijamii kama ilivyokuwa katika karne ya zama za kati za mawe, enzi ambazo wanajamii walikuwa wakifanya mambo kwa kubanwa na mazingira ya wakati huo. Kauli za ‘Kupata ni majaliwa’ Ng’ombe wa maskini hazai’ serkali haituthamini’, ‘sijasoma’, mimi ni mlalahoi ama mlalatabani, 'mkoa wangu ni wa pembezoni,’ ‘kabila letu limesahaulika’, nk, ni kauli za kimaskini, ni kauli za kutafuta visingizio.  Kwakukisoma kitabu hiki utatambua nguvu ya mawazo yako ya kina na utatambua kusudi la wewe kuwepo duniani. Pigania kile ukitakacho usivunjwe moyo na waliochoka kiakili, waliochoka kufikiri, na wasiokuwa na malengo. Na wanaosema ponda mali kufa kwajwa. Go Big or Go Home.
Meshack C. Maganga.








Previous
Next Post »