.

KILIMO CHA MITI KINAVYOZALISHA MAMILIONEA MKOANI IRINGA





          KILIMO CHA MITI KINAVYOZALISHA MAMILIONEA MKOANI IRINGA
Na: Meshack Maganga- (Iringa) Go Big Or Go Home
Makala hii ni matokeo ya mjadala mkali wa WANAMFANIKIO-GOLD, kundi mahusi lililoanzishwa na rafiki yangu Makirita Amani. Siku ya tarehe 24.11.2012 baada ya harusi yangu, nilipigiwa simu na Makirita akiniomba niongoze mjadala wa wanamafanikio jumapili. Niliona ni bahati ya pekee sana maana duniani tupo Wanadamu bilioni 7, na Tanzania tupo Wanadamu zaidi ya milioni 40 hii ilikuwa bahati na fursa mojawapo kuwahi kuzipata.

Siku ya mjadala ilipofika niliulizwa maswali mengi sana, mojawapo ikiwa ni ufafanuzi na maelezo ya jumla juu ya faida ya kilimo cha Miti, swali jingine lilikuwa ni changamoto  katika kilimo cha miti na uchumi kwa ujumla, jingine lilikuwa ni kitu gani kinaweza kusaidia kubadilisha fikra za watanzania kuelewa faida itokanayo na kilimo cha Miti? Mwanamafanikio mwingine alitaka kufahamu ni kwanini ni watanzania wachache sana wanajihusisha na kilimo cha miti? Na akasema nina ushauri gani  kwao na watanufaikaje kiuchumi kupitia kilimo cha miti? 

Nitajibu maswali haya kwa ujumla wake hapa chini. Kwanza: Kilimo hiki cha miti ni (SOMA ZAIDI)
uwekezaji wa muda wa kati na mrefu (middle& long term investments). Kiutamaduni watanzania wengi huwa hawavutiwi na uwekezaji wa muda mrefu. Hata hivyo kama una mpango wa kuwa na “financial freedom” usikwepe kufikiria uwekezaji wa muda mrefu. Waingereza husema “Information is power”. Wengi hawajachangamkia fursa hii kwa kukosa taarifa tu. Tulipokuwa tunaendelea na mjadala ule, nikambukumbuka “Mentor” wangu Albert Sanga, aliposema ‘Wengi wa watanzania wanapenda sana hela za chapchap! Ukitaka umpate mtanzania mpe fursa inayoonesha kuwa fedha itapatikana kesho, wiki ijayo, mwezi ujao na ikizidi sana mwaka ujao. Ukitaka mtanzania asiwe rafiki yako, mweleze habari za kufanya mambo yatakayoleta faida ama fedha kuanzia miaka mitano, kumi, ishirini ama hamsini mbele. Kwanza hatakuelewa na pili atakupuuza’. 

Nilisema kuwa Kilimo cha miti ya mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea, milunda na miti ya kuni na dawa, kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya mazingira. Hapa nchini mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa maarufu inayoongoza kwa misitu mikubwa iliyopandwa na watu binafsi, mashirika ya kigeni na serkali. Miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea pamoja na utengenezeaji wa karatasi na madawa. Hivi sasa kumeibuka fursa nyingine mpya ambapo mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua hewa ya ukaa. Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti halafu ukawa unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae uvune mbao, nguzo ama miti ghafi ya kutengenezea karatasi. Hii ni sawa na kutengeneza pesa ukiwa umelala nyumbani kwako (Making money while sleeping- UNAWEZA KUCHAGUA KUAMINI AMA KUTOAMINI), vile vile unaweza kufuga nyuki na kuendelea kuvuna asali.

Kilimo cha miti, kina faida sana, pengine baadhi ya watanzania wa ndani na nje ya nchi wengi wao hawajabahatika kusikia faida ya kilimo hiki, ama wengi wao wamekisikia na kuzifahamu faida za kilimo cha miti. Wanashindwa waanzie wapi, na ndio maana mpaka sasa wanaolima miti ni watanzania wachache sana, na wale waliojitokeza kulima miti ndio mamilionea wa miaka michache ijayo, Hii ni kwasababu, ukipanda ekari moja ya miti ya mbao ambayo ni jumla ya miti mia sita hadi miatano, ikishakomaa unaweza kuuza mti mmoja kwa bei rejareja shilingi elfu 25 kwa kadilio la chini kabisa, kwa hiyo 25,000 x miti labda mia 5 ni sawa na milioni 12,kwa bei ya sasa. Je miaka 8 ijayo itakuwa shilingi ngapi? Ndio maana pale Mafinga na vijiji vyake, vijana wadogo waliojiingiza kwenye kilimo cha miti ni mamilionea wa miaka ijayo. Na wewe msomaji unanafasi ya kuwa milionea kama utachagua...!

Baadhi ya changamoto nilizo kutana na nazo tangu nilipoanza kilimo cha miti; nikukosa pesa za kutosha hasa kipindi cha kupanda miche mipya kinapoaanza, maana unapopanda miti mpya unatakiwa uwe na pesa ya kutosha. Changamoto nyingine ni tatizo la usafiri, mashamba mengi ya miti yapo nje ya mji wa Iringa, unatakiwa usafiri kilomita nyingi kwa siku mpaka kufika sehemu yalipo mashamba hasa katika wilaya ya Mufindi na Kilolo.

Tulijadilina mambo mengi sana siku ile ya mjadala, msomaji unanafasi ya kuwasiliana na mimi kwa simu ama email ama kupitia mitandao ya kijamii. Na Kabla sijahitimisha makala hii  ninapenda kulisema jambo lifuatalo,kauli za ‘ Kupata ni majaliwa’ Ng’ombe wa maskini hazai’ serkali haituthamini’, ‘sijasoma’, mimi ni mlalaohoi/ mlalatabani’ nk, ni kauli za kimaskini, ni kauli za kutafuta visingizio. Tumia vizuri mawazo yako ya kina ufanikiwe. Jielimishe, soma vitabu vingi, vya mafanikio. Tembelea maduka ya vitabu. Kuna duka moja kubwa sana la vitabu pale Dar, linaitwa ‘The House Of Wisdom’ ukifika pale hata kama usiponunua kitabu, lakini ukisoma vichwa vya vitabu vile, lazima utoke na kitu kitakachobadili maisha yako.  
Achana na mawazo yatakayo kukatisha tamaa,  achana na marafiki wanaokupotezea muda wako, walalamishi, jenga urafiki na waliofanikiwa. Ni mpango wa Mungu ni kukuona wewe  ukishi maisha ya furaha, maisha ya utele na mafanikio katika Nyanja zote za kiuchumi na kijamii na kiroho. Kama kuna kitu kinaitwa bahati, basi asilimia 90 inakwenda kwa wale watafutaji na wachapakazi na wasiokata tamaa.  Ninawatakia mafanikio mema. BINADAMU WENYE MAFANIKIO HAWACHOKI KUTAFUTA- Go Big or Go Home email meshackmaganga@gmail.com   https://www.facebook.com/Fresh-Farms-Trading




Previous
Next Post »