.

Kuna Maisha Baada Ya Maisha Ya Sasa

Na: MROPE Wa MROPE
KUNA MAISHA BAADA YA MAISHA YA SASA:

Wapendwa nimeona niwaandikie kuwakumbusha kuwa hakuna kitu kinasimama vilevile siku zote.

Mambo hubadilika kutokana na nyakati, sheria, taratibu na hali ya uhai kwa wakati husika. Mtu akifa anakuwa na maisha katika pande mbili; maisha ya pale alipo sasa na maisha ya kule anakoelekea.

Mtu akifa anaweza kwenda mbinguni au jehanamu (kwa mujibu wa maandiko ya dini nyingi tunazoabudu kwazo), lakini kwenda mbingu au jehanamu hutegemea aina ya maisha na matendo yake hapa duniani, ikiwa ni mazuri au mabaya, yaliyojaa ujasiri au uoga.

Tena nilipokuwa nikitafakari haya nikaelewa kwa yakini kwamba matendo ya ujasiri au uoga, ukweli au uongo na mengine mengi yanaathiri maisha ya mtu huko aendako na hapa duniani.

Mtu akiwa muoga maana yake hatafanikiwa hapa anapoondoka wala anakokwenda tena mtu muongo hatafanikiwa hapa wala anakokwenda.

Nikatafakari kwa namna ya majukumu tuliyonayo juu ya familia zetu na wale wategemezi wetu, hapo tena nikaona ya kuwa hata mtu akifa majukumu yake hapa duniani huendelea.

Fikiri kuhusu wale wanaokutegemea sana leo, kifo chako kitafanya yale wanayoyategemea kwako kukoma? Kama wanatarajia uwanunulie chakula, je watakoma kuhitaji chakula mara baada ya wewe kufa? Basi katika kutafakari huko nikasema imempasa mtu kufahamu kuwa kuna maisha baada ya maisha ya sasa na imempasa kila mtu kujiandaa vyema kwa maisha hayo ya pande mbili.

Nikazidi kutafakari nikaona tena ya kuwa nyakati hubadilika na nyakati zinapobadilika maisha nayo hubadilika kamwe hayasimami vile vile, hapa nikatamani ujiulize, "baada ya nyakati hizi kuna nyakati nyingine za maisha mengine ya kupanda au kushuka

Mimi nitakuwa kundi lipi?". Nikatafakari mabadiliko ya sheria na utamaduni nikaona nayo yanaathiri maisha ya watu katika kupanda au kushuka.

Hapo tena nikaona ya kuwa maisha yanapanda au kushuka kutokana na mabadiliko na kuhusu wapi mtu awepo ni uamuzi wake.

Nikajiuliza kwa mfano wa mtu aliyemiliki baiskeli miaka ya 1980 kwamba alionekana ni mtu mwenye mafanikio lakini zinapokuja nyakati ambazo teknolojia ameleta piki piki na magari mengi yule tajiri wa baiskeli anakuwa upande upi kwa sasa.

Hebu jiulize yule aliyetikisa mtaa wenu kwa kumiliki siemens ya dole au siemens mayai leo amekwenda kwenye ipad au yupo kwenye nokia ya torch? Basi nikafahamu ya kuwa kuna maisha baada ya maisha ya sasa na katika maisha hayo kuna mabadiliko yanatatokea lakini sijui kama yatakupeleka juu au chini, kuzuri au kubaya na kutokana na hilo nikaona nichukue simu yangu nikuandikie huku nikijiuliza haya ninayotafakari na kutenda leo yatanipeleka juu au chini? Lakini nina hakika ya maisha niliyoyachagua baada ya maisha haya maana maisha yajayo ni matokeo ya uchaguzi wa sasa.

Che Mrope Wa Mrope, Mbeba Maono (fb page) 0766656626/0787641417/0715366010

Previous
Next Post »