.

Usitarajie Kuwa Na Kesho Bora Kama Unawaza Mazagazaga Leo



Na : MROPE WA MROPE. Iringa

Maisha yetu hivi yalivyo ni matokeo ya kuwaza hii maana yake ni kuwa yote tuyaonayo ni matokeo ya
mambo yaliyoishi katika vichwa vya watu na kisha yakatendwa.
Hii maana yake ni kuwa yapo mawazo yaliishi vichwani mwa watu na yakafia humo vichwani mwao. Yote tuyaonayo ni mawazo ya watu waliowaza vizuri na kuthubutu kutenda, vivyo hivyo mengi ambayo hayapo ni matokeo ya watu waliochagua kuwaza mambo manyonge au waliowaza bila kutenda.
Kwa hiyo unapowaza mabaya utatamka mabaya, utatenda mabaya na utapokea matokeo mabaya. Kama unaamini kushindwa utatamka kushindwa na utatenda kinyonge na kushndwa vibaya. Kwa hiyo ili ushinde unapaswa kuwaza mawazo hai na si mawazo mfu.
Kama unawaza majuto yaliyopita usitarajie kuwa na mema yajayo. Kuwaza majuto kutapelekea utamke majuto na utarajie kupewa pole na upate faraja kwa unyonge wako kisha upate sababu ya kulala kwa unyonge badala ya kutenda.
Ili kupata matokeo lazima utafakari yaliyo mbele kwa kina tena iwe mbele kweli kweli maana huko mbele ndiko yaliko maisha yako yawe mazuri au mabaya lakini uzuri au ubaya huo hutegemea nini unatafakari leo. Hapa kuna kutafakari na kisha kutamka na kutenda. Kutamka na kukiri ni muhimu sana maana kinywa huumba na hiyo ndiyo sababu mimi naamini mawazo lazima yaunganishwe na matamshi kisha kutenda.
Kwa hiyo kuwaza peke yake hakutoshi bali unapaswa kutamka ili uumbe, upate picha, upate ujasiri na uone deni la kutenda linalokukabili. Kutotamka hukupa faraja na kujiona huna deni la kutenda chochote. Kuna watu wanasema sitatamka  kwa kuwa nikishindwa nitaiweka wapi sura yangu. Huyo hatatamka na hatatenda maana ameshajipatia hifadhi ya uzembe.
Unaweza kutamkia moyoni mwako kisha ukafungua kinywa na kujitamkia mafanikio kila unapotoka nyumbani na kila unapoelekea utendaji wa jambo lolote ulilojpangia.
Kujitamkia huku huwa na matokeo murua katika ulimwengu wa roho. Unaweza kumtamkia mtu ambaye ana mawazo ya kushinda ili awe anakusukuma kutenda maana mafanikio yanahitaji msukumo pia. Lakini ili uwe na matokeo sahihi lazima utafakari kesho, utamke kesho na utende leo. Bado unatafakari jana? Kama ndivyo kesho yako umemuajiri nani aitafakari?
ALOYCE MROPE, Che Mrope Wa Mrope (fb) Mbeba Maono (fb page) 0766656626/0715366010/0787641417


 
Previous
Next Post »