Na: MROPE Wa MROPE
Tufanye mambo
yote tufanyayo lakini tukumbuke mwisho wa siku tunawajibika mbele za
Mungu ambaye ndiye muumba wetu. Kwa mantiki hiyo basi
ni vyema tunapotafuta mafanikio tusitafute mafanikio ili "kuwashushua"
wakina fulani au ili kujionesha na kupata sababu ya kujisifu ati sisi ni
bora sana kuliko wengine. Ninajua kwa yakini kila mtu anapotafuta
mafanikio anasukumwa na
jambo fulani moyoni mwake lakini msukumo wowote
wenye dhamiri ovu ni ngumu kufanikiwa au mafanikio hayo humuondolea mtu
amani ya moyo.
Aidha siri kuu ya mafanikio ni dhamiri
ya kuwafikia watu wengi bila kuwabagua kwa namna yoyote maana kila mmoja
yupo namna alivyo kwa makusudi maalumu hivyo kutafuta mafanikio ili
kumnanga fulani au ili uonekane bora ni janga la safari ya mafanikio
yako.
Mara nyingi nimekuwa nikitoa mfano wa Mfalme
Suleimani (Solomoni) ambapo alipotokewa na Mungu na kuulizwa amtendee
nini? Yeye alijibu kwa unyenyekevu, "Naomba hekima ya kuongoza watu
ulionipa". Wangapi leo wangejibu hivyo? Wengi wangesema, "Unajua Mungu
hawa watu ulionipa ni wengi tena ukikutana nao wanapenda sana kuombaomba
nami sina pesa kwa hiyo nijaze miutajiri".
Mafanikio
yoyote yana siri kubwa na Mungu huwa anamuinua mtu ili kuinua wengine
wakiwepo wale ambao hawakupendi na wanakuchukia kwa bidii sana. Yusufu
alipata kuwa waziri kwa mfalme ili awasaidie chakula nduguze (wakiwepo
wale waliomuuza) wakati ule wa njaa.
Kwa hiyo ikiwa mtu
yoyote ana dhamira na mafanikio makubwa lazima awe na dhamiri moyoni
kwamba akifanikiwa ataitazamaje jamii yake.
Kila mmoja
wetu anajijua siku ya kufanikiwa kwake atatazama vipi wale
"aliowafunika". Kuna wengne hawaioni kabisa jamii kwa mema au mabaya ila
wanajiona wao tu katika ulimwengu wao wa ubinafsi.
Mungu
humpa vingi mmoja ili kufikisha wengi ili nao wakifanikiwa wajifunze
kwa mfano huo lakini kujiona peke yako ndiko kunazuia mafanikio ya
wengi.
Tukumbuke kabla ya kufikiwa mafanikio yetu
dhamiri zetu hujaribiwa na Mungu na hata wale wa mlango wa nyuma
hujaribiwa pia kwa kutakiwa kushirikisha damu za wawapendao kuwa
kinywaji cha mapepo.
Mafanikio yoyote yadumuyo ni yale yanayogusa maisha ya wengine pia na sio kuwatesa au kuwadhihaki.
ALOYCE MROPE, Che Mrope Wa Mrope (fb) Mbeba Maono (fb page) 0787641417/0766656626/0715366010
Sign up here with your email