.

Maisha Hayana Rimoti, Kusema Utaibonyeza, Amka Na Utende.


Na: MROPE wa MROPE- Iringa 

Kila binadamu chini ya jua ana uhuru wa kuchagua; kufanikiwa au kutofanikiwa. Mafanikio hayamfuati mtu shida tumezaliwa nazo maana sote tulizaliwa tukiwa watupu na mengine yote tuliyonayo yawe mazuri au mabaya tumeyapata tukiwa hapa duniani. Uamuzi wa
kufanikiwa au kutofanikiwa upo katika matendo yetu ambayo ni mazao ya fikra na matamshi yetu. Hakuna binadamu ambaye hana matendo, kila sekunde tunatenda jambo fulani la lazima au si la lazima, baya au zuri.

Haikwepeki lazima kila binadamu atende; atake au asitake. Mafanikio yetu au kushndwa kwetu kupo katika matendo hayo maana kila sekunde mtu hufikiri, hutazama, husikiliza, hutembea, huongea, n.k. 

Katika matendo hayo ndiposa mtu hutenda kwa faida au kwa hasara, hujenga au hubomoa, hufikiri kulaani au kubariki, hutazama matambiko au mbinu za mafanikio, husikiliza mema au maovu n.k. Katika uchaguzi wa nini tutende na nini tusitende ndipo ilipo njiapanda ya kushinda na kushindwa.
Kwa namna hii imekupasa kujiuliza katika matendo yako unayotenda mangapi yanakuinua na mangapi yanakushusha? Mangapi unatenda kwa ajili ya kesho yako na mangapi unatenda kwa ajili ya kesho ya wengine huku ukiamini unaitendea haki kesho yako? Ukitafakari vizuri utagundua wapo watu wanamaliza hata wiki nzima hawajatenda matendo yanayojenga kesho yao ili kuibomoa au kuisusa. 

Jiulize pale unapobishana kwa jazba kuhusu nani mkali kati ya Mesi na Ronaldo, Man Pacquiao na Mayweather, Ali Kiba na Diamond n.k unakuwa umeijenga kesho yako kwa namna gani? Jiulize unapolalamika kutaka uonewe huruma unakuwa umeijenga kesho yako kwa mtindo gani? Kuna wakati watu wamekuwa mashabiki wa mambo yasiyowahusu toka mwanzo mpaka mwisho wa wiki, Januari mpaka Desemba bila hata wao wenyewe kujijua.
Fikiri upya kuhusu matendo yako. 

ALOYCE MROPE, Che Mrope Wa Mrope (fb), Mbeba Maono (fb page) 0787641417/0766656626/0715366010
Previous
Next Post »