.

Mnyororo Wa Utajiri (Sehemu Ya Tatu)


 
Na: Albert Sanga. Iringa
Maamuzi ya kufanikiwa yanahitaji sana utafsiri ndoto zako ili ujue kiwango unachotakiwa kupambana. Ikiwa malengo yako makubwa ni kumiliki gari na nyumba, ujue upiganaji wako hauwezi(SOMA ZAIDI)
kufanana na mwenye malengo ya kumiliki shule kubwa. Hata hivyo niseme pia kwamba hata yule alielenga kuwa jambo kubwa maishani mwake ni gari na nyumba, pia inategemea anataka gari aina gani na anataka nyumba ya aina gani.kama mtu anakusudia maisha yake yote walau apate Toyota passo na nyumba ya chumba sebule chumba; mtu huyu upambanaji wake hauwezi kulingana na mtu ambae amepanga kumiliki Hammer, V8 n.k au aliepanga kujenga kitu cha ghorofa..
Anaewaza passo na nyumba ya chumba sebule chumba anayo haki kikatiba (kwa katiba ya uchumi) kuridhika na mshahara ama hali ya kipato alichonacho. Lakini ukifika hatua ukawaza hammer na kitu cha ghorofa, huwezi kutulia kabisa na kipato unachopata. Kwa nini?Kwa sababu malengo uliyojiwekea yatakuwa yanakulaza macho kimawazo.
Nilikwambia wiki iliyopita kwamba, kinachotutofautisha kiuchumi sio vipato tunavyopata, bali ni namna tunavyofikiria kuhusu wengine.kadiri unavyowafikiria wengine kwa wingi ndivyo unavyokuwa na nafasi ya kufanikiwa kwa kiwango kikubwa. Nitakupa mfano: mtu anaewawazia watoto wake wasome shule za kimataifa, akili yake ya kutafuta hela haiwezi kufanana na yule alieamua watoto wasome kwenye shule za kayumba. Una watoto wawili, mmoja ada milioni 2 mwingine ada milioni 3 mshahara wako ni milioni 1 na pointi; hakika nakwambia kuwa huwezi kutulia kuridhika na mshahara, utapambana.....
Mnyororo wa utajiri unataka kuwa ili ufanikiwe ni lazima ufanye mambo mawili:1. Utatue matatizo yanayokupata
2. Kama huna matatizo basi tengeneza matatizo. Hakuna mtu anaeweza kuwa na sababu ya kutafuta mafanikio, isipokuwa kumekuwepo tatizo..
wiki iliyopita nilikupa ile push power na pull power. Ilivyo ni kwamba
1. Push power: matatizo/changamoto vimekupata, huna namna nyingine isipokuwa kukubali kufa ama kupigana (matatizo yamekukuta)
2. Pull power: huna matatizo ama changamoto kubwa ya kukufikirisha, lakini unaamua kuyatafuta matatizo ili upate nguvu ya kupambana.
kama unasomesha mtoto shule ya msingi ya "wazalendo" na ikatokea mtoto amekosa mchango wa mwenge shuleni na wewe huna hela, hilo tatizo limekujia, huna namna isipokuwa kupambana...
Hebu tuache mfano wa mchango wa mwenge, maana unaweza kuona ni kitu kidogo. Chukulia kwamba umetokea umeumwa ama mtu wako wa karibu anaumwa na inabidi apelekwe nje kwa matibabu na wewe huna hela; wala hakuna kwa kupata msaada; hapa ndipo unatakiwa eidha ukubali kifo ama upambane (push power).
Lakini chukulia tena kwamba umeamua kwa hiari kuwa ni lazima muda fulani uende nje kufanya "medical check up" ya kawaida kuangalia mwili ukoje; itakubidi utafute hela ili uende sio? Hii tunasema umeamua kutengeneza tatizo na sasa unahangaikia hela push power mara nyingi isipounganishwa na pull power huwa haiwezi kumfanikisha sana mtu.
Fikiria kwa push power umepambana, na kufanikiwa kupata fedha za kwenda kutibu/kutibiwa na ukarudi ukiwa umepona. Ni rahisi kufika na kutoendelea kupambana kwa sababu kilichokusukuma upambane na kutafuta hela kimeshaisha... lakini chukulia kwamba umeenda kufanya check up ya kawaida na ukarudi; kwa kuwa tatizo hili (maamuzi ya kwenda check up), ulilitengeneza mwenyewe, ni rahisi kuliendeleza na kulikuza.
Yaani unaweza kusema kuanzia sasa, kila mwaka nitakuwa ninaenda nje kufanya check up kila mwaka(umeliendeleza tatizo). Pia unaweza kusema sitakwenda peke yangu, bali nitakuwa nikiambatana na familia yangu yote(umelikuza tatizo). Kama ukienda mwenyewe ulikuwa unatumia dola 5,000 utalazimika kutafuta fedha zaidi ili zitoshe za kwenda wewe, mke/mme na watoto.
Waangalie wale watu ambao huwa wananyanyaswa sana na wenye nyumba! Kinachowalazimishaga (nimetumia kibantu kidogo) wajenge nyumba ni push power, kwamba hawana namna isipokuwa kupambana wajenge zao ili adha za wenye nyumba ziwaishe.
.Lakini push power isipofuatiwa na pull power, ndio unaweza kuona mtu kahamia kwenye pagale lake, hata madirisha hajaweka, miaka inapita yumo humo humo, pagale haliishi yupo tu hadi anazeeka..unajiuliza ile nguvu na hasira alizotumia kujenga nyumba hiyo baada ya kukerwa na mwenye nyumba, zimepotelea wapi? Jibu ni rahisi  sanakuridhika!...Nasisitiza sana pull power kwa sababu ni nguvu iliyokosekana kwa wengi hasa wafanyakazi walioajiriwa. Kama kuna jambo linawafanya wafanyakazi wasipige hatua za kimaendeleo zaidi ya walizo nazo, basi ni kurishika na woga.
Nilikwambia wiki iliyopita kwamba ukiona mtu karidhika ujue sio kwamba mshahara wake unatosha, la hasha! bali ni kwa sababu ana malengo madogo.
Na matokeo ya malengo madogo ni ubinafsi.Ni ubinafsi kwa sababu mtu anafikiria nyumba ya kuishi yeye pekee, anafikiria gari la kutembelea yeye pekee, akijitahidi sana atawafikiria kina wifi na kina dada zake kidogooooooo...sisemi kwamba kujifikiria wewe na nduguzo ni vibaya, ila ninataka kusema kwamba ukijitahidi kuwafikiria zaidi ya hao, unakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa zaidi....
unapoanza kuwafikiria wengine zaidi ya wale ambao ni wajibu wako; ndipo tunasema unakuwa ukitengeneza matatizo. Kufikiria kujenga nyumba ya kupangisha maana yake umewafikiria wale ambao wanahitaji makazi.
Kama ungeamua kutulia na kunywa juisi kwenye nyumba yako hiyo moja bila kuwawazia hawa waitwao wapangaji; ina maana usingekuwa na hili tatizo. Kwa nini ninaliita ni tatizo; ni kwa sababu itakubidi uanze kuhangaika kutafuta uwanja, uhangaikie ramani hapo bado hujaumiza kichwa kwa kupata hela na sijataja mchakamchaka wa kukimbizana na mafundi saiti...
Hili la kutafuta matatizo ili uyatatue, wengi huwa wanaona ni michosho ndio maana huamua kutulia walipo. Huwezi kufanikiwa kiuchumi kwa "kumaintain status"(nimeongea kimishenari kidogo). Wenzetu walisema meli iwapo imetia nanga baharini inakuwa salama, lakini kutulia bandarini sio lengo la kuundwa kwa meli. Meli imeundwa ikapigane huko kwenye mawimbi. Ndivyo ilivyo kwa binadamu kiuchumi....
Na utashangaa kwamba watu wanaofikiria wengine, wanaotengeneza na kutatua matatizo ya wengine ndio ambao huwa wanapata na kumiliki vile ambavyo wengi wanavitamani....
Hebu tuwe wawazi; ni akina nani wanamiliki magari ya gharama na majumba ya kisasa?
wakati unaangalia jibu la hilo, jiulize tena, ni nani asiependa magari ya gharama na nyumba za kifalme? Bila shaka ni wote, sio?Ninachotaka ukione sio haya magari na majumba, la hasha! bali nataka uone kuwa: wanaojishughulisha kufikiria namna ya kutatua matatizo ya wengine ndio wana nafasi kubwa ya kufanikiwa zaidi ya ukawaida na hata kuufikia mnyororo wa utajiri....
Muelewe kwamba utajiri ni kile kinachobaki baada ya mahitaji na matakwa yako kutimia kwa 100%. Pia ninapenda muelewe kwamba kuna kipindi cha mpito ambacho mtu huwa anakuwa safarini kuelekea kwenye utajiri. Hapa wapo watu wengi, na mbeleni nitakwambia mambo ya kufanya katika kipindi hiki cha mpito, ili usifie njiani pasipo kutajirika.
Nataka nirudi kuleee kwa siku ile nilikokueleza aina tatu za watu kiuchumi (waajiriwa, wafanyabiashara na wasio na kazi), ili niunganishe na namna pull power inavyoweza kukuweka katika uhuru wa kifedha. Kabla ya kwenda huko naomba nikupe kwa ufupi makundi matatu ya watu na vipato(itakusaidia kuelewa ninachotaka kukuingizia kichwani)....
utaona kuwa fukara (anaishi kwa madeni), masikini(anaishi pasipo akiba), tajiri(ni mtu mwenye akiba muda wote. Kuna watu wanalipwa milioni 2 ni masikini na wengine wanalipwa laki 2 ni matajiri!Kwa leo naomba niishie hapa, nitaanzia hapa wakati ujao, asanteni kwa kunifuatilia. Mbarikiwe!
Previous
Next Post »