.

Mnyororo Wa Utajiri (Sehemu Ya Pili)

 Na: Albert Sanga. Iringa
Ukitaka kufanikiwa ambatana na waliokusudia kufanikiwa. Kundi hili naamini tumekusanyika watu tuliodhamiria kufanikiwa, kwa hiyo ukiwa hapa uwe na uhakika kwamba upo mahali sahihi kabisa.
Ninaendelea na mada yangu ya mnyororo wa utajiri, sitakuwa na wasaa wa kurudi nyuma isipokuwa kwa ufupi ni
kwamba nilikueleza kwamba mnyororo wa utajiri ni uhakika wa wewe, watoto wako na wajukuu zako kuwa safi kiuchumi kutokana na bidii, misingi na mambo utakayoyafanya sasa na hapo baadae.
kimsingi ni kwamba una aina mbili ya maisha ambayo watu wanaishi
1. Kufanya kazi kwa ajili ya kujitosheleza wao binafsi
2. Kufanya kazi kwa ajili ya kuwatosheleza wengine. Nikiongeleza kujitosheleza namaanisha kuwa mtu anafanya kazi kwa ajili yake, watoto wake na pengine nduguze basi!
Tunapoongelea mnyororo wa utajiri tunakusudia ile namba 2 ambapo mtu anafanya kazi kwa ajili ya kuwatosheleza wengine. Swali la kujiuliza ni hili, je, picha gani inakujia kichwani kila unapopata mshahara? (kama umeajiriwa)
Je inakuja picha ya kulipa madeni, kulipa kodi, kununua chakula, halafu hela inakata kabla picha nyingine haijaonekana? Kama wewe ni mfanyabiashara, mjasiriamali ama huna ajira, je, nini kinakuja kichwani mwako unapoitazama kesho yako?Kama unaiona familia yako pekee huko ni kuishi ama kupanga kuishi kwa kujitosheleza na kama unaona picha zaidi ya hapo basi huenda unafikiria wengine.
Mtu mwingine ataniuliza, kuna haja gani nifikirie kuwatosheleza wengine? Ama atanieleza kuwa kila mtu atajijua kivyake! Siri iliyopo ni kwamba, hakuna mtu anaeweza kufanikiwa isipokuwa amewafikiria wengine.
Muuza genge anapata faida kwa sababu amewafikiria wanaohitaji mahitaji ya nyumbani. Mwenye basi anapata faida na maendeleo kwa sababu anawafikiria wenye shida ya kusafiri. Mama Ntilie asingepata faida isipokuwa amewafikiria wenye njaa.
kwa maana hii utaona kwamba mafanikio ama niseme maendeleo ni matokeo ya kujituma ama kulazimishwa kuwafikiria wengine. Nimesema kujituma ama kulazimishwa kuwafikiria wengine kwa maana kuwa mafanikio ni ama uvutiwe kufanikiwa au ulazimishwe kufanikiwa.
Ndio! mafanikio yeyote ya maana(makubwa) hayaji mpaka uwe umevutiwa kufanikiwa ama umelazimika kufanikiwa. Kuna wakati ambapo unafanikiwa kwa kuvutiwa na waliotangulia kufanikiwa na kuna wakati shida na matatizo vinakulazimisha kufanikiwa!
Hii dhana ya kufanikiwa kwa kujituma/kuvutiwa na kufanikiwa kwa lazima kwa kimishenari wanasema push-pull power. Mifano ya hii dhana unaweza kuipata kwa makabila mawili, wakinga na wachaga. (Wachaga na wakinga wenzangu msimaindi kwa kuwa nimewataja)
Sehemu kubwa ya Wachaga  huwa wanadhamiria kufanikiwa kutokana na kuiangalia mifano ya waliowatangulia. Kwao (walio wengi) kinachowafanya kupambana na maisha sio ugumu wa maisha uliopindukia, bali ni kiu ya kufika kukubwa zaidi ya ama sawa na waliomtangulia. Historia ya wakinga ipo tofauti kidogo. Kwao hawa dini ilichelewa, elimu ilichelewa; kwa hiyo familia nyingi zilikuwa katika umasikini uliopindukia.
Kilichokuwa kikiwafanya wakinga wotoke huko milima ya ukingani kwenda kutafuta vibarua kama manamba kwenye mashamba ya chai, mkonge, n.k ilikuwa ni maisha magumu yaliyokuwa yakiwatandika .
Wengi wao walikuwa hawana namna, ni eidha wabaki huko Ukingani na wafe kwa njaa na maisha magumu ama watoke na kwenda kutafuta ili waishi! Hii ya wakinga ndo inaitwa push power na ile ya wachaga inaitwa pull power.
kwa kusema hivyo haimaanishi kwamba hakuna wachaga wanaotoka kwa push power, ama wakinga wanaotoka kimaisha kwa pull power, isipokuwa nimesema sehemu kubwa ya wachaga na nikasema hivyo kukuonesha namna wakinga wengi walivyotoka kihistoria .Pointi yangu sio kutaka uwajue wachaga ama wakinga, bali nataka uone mazingira mawili yanayoweza kukutoa kimaisha.
1. Kama unadhani umeshafika kimaisha, huna namna itakayokutoa hapo kwenda mbele isipokuwa umetumia pull power, yaani kwa hiari yako uwatazame walio mbele yako na udhamirie kufanya sawa ama zaidi yao
2. Kama unapitia kwenye kipindi kigumu kimaisha, ni muda mzuri wa kuamua ikiwa ufie hapo ama uinuke na kupambana
Hata hivyo katika mazingira yote mawili hapo juu, no. 1 na no. 2, msingi wa kutoka hapo ni wewe kuwafikiria wengine. Kwa mfano kama unadhani umeridhika, labda kwa sababu una kazi nzuri na mshahara mkubwa ambao unatosha kusomesha watoto wako na kujihudumia na wale wanaokuzunguka; ili utoke hapo itabidi uwafikirie wagonjwa ili upate hamasa ya kujenga hospitali, uwafikirie watoto ili upate hamasa ya kujenga shule yako, uwafikirie yatima ili uanzishe kituo cha kuwalea, uwafikirie abiria ili ununue mabasi ama ndege, na orodha inaendelea.
Unajua kinachowafanya watu waridhike na kuona kana kwamba wameshafika na kumaliza katika maisha ni kwa sababu ya mawazo na ndoto za kibinafsi. Ukiwa na ndoto kubwa na mawazo ya kuwafikiria wengine, huwezi kufika mahali ukasema hela zimekutosha ama ukapumua eti ukajiona umefika...
kama wewe ni mwalimu jaribu leo kuwaza kumiliki shule yako uone kama utaridhika na huo mshahara wa ualimu. Kama wewe upo kwenye shirika la kimataifa, jaribu kuwaza kufungua shirika lako mwenyewe siku moja huko mbeleni, uone kama mshahara na marupurupu wanayokupa yatakuzuzua.
Mimi huwa nashangaa hata ninapomkuta daktari amebweteka na kuridhika na kibarua chake, moyoni huwa najua kwamba huyu daktari karidhika kwa sababu kichwani mwake hakuna hospitali kubwa na ya maana.Nafahamu kuwa kundi kubwa la watu lipo hapa no. 1 moja, ambapo wameridhika na hatua walizofikia, wanapumua, wanajiona wamefika.
Hata katika sababu no. 2 ya kutakiwa kukufanya ufanikiwe, yaani push power; uhalisia ni kwamba kufanikiwa kwako kutategemea namna unavyowafikiria wengine. Kama ilivyokuwa kwa Wakinga, hatua ya kwanza unapokwama na unapokuwa huna namna nyingine ni kufikiria wanaokuzunguka.
Unafikiria: ni kweli maisha yamenipiga, lakini nikibaki hapa bila kuinuka na kupambana itakuwaje wanangu, itakuwaje mke wangu, itakuwaje wadogo zangu n.k
Previous
Next Post »