Na: Meshack Maganga- Iringa
Ndugu zangu, Wito wangu sikuzote umekuwa ni kutumia muda wangu mwingi kuwasisitiza
rafikizangu, ndugu na wadau wengine wote, kuangalia uwezekano wa
kuzitambua fursa mbalimbali zilizopo kwenye mazingira yetu. Hakuna
sehemu yeyote ya dunia ambayo haina fursa na ambayo imesahaulika, bila
kuwa na fursa za kuitosha jamii, isipokuwa macho yetu ya
ndani hayazioni
fursa hizi. Vitakubwa tuliyonayo ni ya kupambana katika kuondoa
mitazamo hasi iliyomo kwenye vichwa vyetu tuweze kuziona fursa hizo.
Tumezungukwa na fursa (Neema ya Mungu) ni ajabu kumsikia mtu anaeishi
Morogoro ama Iringa halafu hafahamu kilimo cha vitunguu, hafahamu kama
kuna kilimo cha mitiki, ama haamini kwamba kuna watu wameshafikia kwenye kilele cha mafanikio
kwa kujishughulisha na kilimo cha matembele, ufugaji wa samaki na mambo
mengine madogomadogo ambayo waliopitapita vyuoni wanadia kwamba ni hizo
ni kazi za watu duni waliokimbia ‘umande’.
Mtu anaishi Dar hana taarifa
kwamba Bagamoyo ama Mkuranga, kuna kilimo cha mitiki, Vitunguu, nyanya,
mihogo nk. Ajabu yingine kuna wanaoishi Iringa, lakini hajawahi
kujifunza kilimo cha miti angalau wapande hata nusu ekari ya miti na
huyu bado atakuwa anaitupia serkali lawama kwamba haimjali, swali,
unataka serkali ikujali wakati unalala na kushinda facebook kupiga
majungu? Badilisha mtazamo wako.
Watalaamu wa Elimu ya utambuzi na mawazo ya kina kama akina Paul Msatu
wanasema kwamba, Sisi sote ni mawazo yetu, kuishi kwetu ni mawazo yetu,
mafanikio yetu ni mawazo yetu, uchumi wa taifa letu ni mawazo
yetu.Utamaduni wa taifa letu ni mawazo yetu. Ukweli wa maisha yetu,
mafanikio yetu, upo ndani yetu katika mawazo yetu. Uwezo mkubwa
unaotutofautisha kati yetu sisi na viumbe wengine upo katika mawazo
yetu. Tabia zetu, matendo yetu, kuamini kwetu na zaidi kuishi kwetu ni
kuwaza kwetu. Mafanikio yote duniani, utajiri wote duniani na hata
umaskini wa mwanadamu vyote vimeanzia katika mawazo na mitazamo yake juu
ya maisha.
Hakuna mtanzania asiyefahamu matumizi ya miti, labda kwa kukumbushana
tu, baadhi ya matumizi ya miti ni kama vile, mbao, nguzo, chakula,
kilimo mseto, hifadhi ya vyanzo vya maji, kurutubisha udongo, kulisha
mifugo, kuboresha hali ya hewa, kuni, mkaa, dawa na mapambo.
Kosa tunalolifanya na kusababisha tuzipoteze fursa za mafanikio, hata
kama zinachukua muda mrefu ni mtazamo mbaya wa kufikiri kwamba fursa za
mafanikio zipo nje ya maeneo tunayoishi. Ifahamike kwamba, fursa za
mafanikio ya kiroho na kimwili hutafutwa kwasababu haziwezi kujileta
kwasababu zina tabia ya kujificha. Baadhi ya fursa hujileta zenyewe
kwetu na kama haziji upande wetu ni vizuri tukazifuata kwenye maeneo
yanayotuzunguka.
Kuna watanzania ambao wanafikiri upandaji wa miti ya mbao na nguzo ni
mkoani Iringa pekee, ninapenda kutoa wito kwa watanzania wenzangu kwamba
unaweza kupanda miti popote pale ulipo, (Tanzania Tree Seed Agency-
TTSA) wametoa mwongozo wa upandaji miti kwa kila kanda, na kila mkoa,
hakuna mkoa Tanzania ambao hakuna miti. Ukiwa Mwanza, Singida, Mbeya ama
Kigoma na kwingineko panda miti inayostawi eneo hilo na faida yake
utaiona. Faida ya miti huonekana baada ya miaka mingi 8-10 na kama
huwezi kusubiri miaka hiyo ni bora ufanye jambo jingine.
Ili kupata faida za miti hakuna budi kufanya uchaguzi sahihi wa miti ya
kupanda kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa. Mfano miti inayofaa kwa
kivuli ipandwe sahemu zinazohitajika kuwa na kivuli na iwe ni ile
isiyopukutisha majani yote msimu wa kiangazi, miti ya kilimo mseto iwe
ni miti yenye mizizi inayokwenda chini zaidi ya sentimeta 50 na iwe
inayorutubisha ardhi, yenye kivuli chepesi na inayofaa kwa malisho. Miti
ya mapambo iwe na maua ya kuvutia, isiwe na mizizi inayotambaa mbali na
isiwe inapukutisha majani yote wakati wa kiangazi.
Hakikisha kuwa unapata mbegu bora za miti kwa ajili ya kuzalisha miche
ya kutosha kupanda katika maeneo utakayoyaandaa. Mbegu hizi bora za miti
zinapatikana kutoka Wakala wa Mbegu bora za miti (Tanzania Tree Seed
Agency- TTSA). Ni Wakala wa Serikali ya Tanzania ambao ni idara iliyo
chini ya Wizara ya Mliasili na Utalii. TTSA ina uzoefu katika
takinolojia ya mbegu bora na safi za miti. Wakala pia unatoa mafunzo ya
muda mfupi (majuma 2) yanayohusu uvunaji mbegu hasa kwa wale ambao
hawawezi kununua mbegu kutoka TTSA, Wakala wa mbegu.
Kitalu hujengewa banda ili kuwe na kivuli kwa mbegu zinazoota. Kibanda
kinaweza kuwa cha majani au fito zenye kipenyo cha sm 2 yaliyoshonwa kwa
kamba kiasi cha meta 2 juu ya kitalu kwa kukiegemeza kwenye nguzo
zilizofungwa pamoja na fito. Pande zote za kitalu ziachwe wazi ili hewa
ipite kwa urahisi.
Inapendekezwa na baadhi ya watalamu wa kilimo cha miti kuwa - wakati
miche michanga imeanza kuota majani ya kwanza, yango’lewe kwenye vitalu
na ipandikizwe kwenye viriba kama ifuatavyo: kishimo kirefu zaidi kuliko
mizizi ya miche kitengenezwe kwa kijiti ili mizizi isije ikapinda
kuelekea juu. Pia kishimo kiwe na upana wa kutosha, vinginevyo mizizi ya
pembeni itashika ukingoni na kupinda juu wakati mche ukiingizwa.
Gharama ya kuanzisha bustani ya miche inatatofautiana kulingana na
mahali bustani ilipo. Ifahamike kwamba, unaweza kuanzisha kitalu cha
miche popote ulipo Tanzania, kuna wanaofikiria kwamba, uanzishaji wa
kitalu cha miche lazima iwe Iringa, ama Lushoto, Morogoro ama
Njombe,unachotakiwa kukifanya ni kubadilisha mtazamo. Wale wanaoishi Dar
mtakuwa mmeshaona baadhi ya watanzania wenzetu pembeni mwa barabara
wakiuza miti, ukiwa na akili ya kutoona mambo huwezi kuwaona.
Ninakuhakishia popote pale ulipo unawezakuanzisha kitalu na ukauza
miche, ikakuweka mjini. Kwa upande wa Iringa hasa kijiji tunachofanyia
kazi sisi, gharama ya kuanzisha bustani yenye miche 100,000. Inakadiliwa
kufikia shilingi milioni 4, hii inajumuisha, gharama za udongo kutoka
mstuni, viriba, dawa za kuzuia wadudu, vifaa vya kujengea kitalu, mbao,
misumari, vifaa vya kufanyia kazi, kama vile matoroli, mipira ya maji,
watering can, majembe nk. Mbengu, na usimamizi kwa miezi mitano na banda
la ofisi.
Miche huwekwa chini ya kivuli kama kile cha kitalu cha mbogamboga.na
umwagiliaji wa maji hufanywa mara kwa mara kutegemea na hali ya hewa ya
sehemu kitaulu kilipo.
Muda wa kupeleka miche shambani unapokaribia kivuli huondolewa polepole
aidha kw kupunguza majani kwenye kibanda au kwa kuondoa kibanda kwa
muda mrefu zaidi kila siku mpaka miche itapoweza kustahimili jua la moja
kwa moja. Upunguzaji wa unywesheaji, dhidi ya mahitaji ya miche itumike
ili “kukomaza” miche tayari kwa kupanda shambani. Viriba visogezwe mara
kwa mara ili mizizi inayojitokeza chini ikatike. Njia nyingine ni
kuinua viriba na kukata mzizi mkuu chini kwa kutumia kisu kikali.
Viriba vinaweza kupaliliwa kwa kutumia kijiti chenye ncha kali au
kutumia mkono. Miche hiyo huchuka miezi 4 na kuendelea kuikuza tangu
siku ya kuipandikiza kutegemeana na miti inayohusika.
Uandaaji wa kitalu cha miche, unatakiwa ufanywe kwa makini sana,
usipokuwa makini utaotesha miche isiyokuwa na tija, ukumbuke kwamba,
uuzaji wa miche inaweza kuwa moja ya njia rahisi sana ya kujipatia
kipato popote pale ulipo, kwa mfano, kama umeotesha kitalu cha miche 5
(elfu tano) ya mbao, kuni,dawa ama nguzo ama miti ya mapambo na kati ya
hiyo miche ukabahatika kuuza miche elfu tatu kwa bei ya shilingi mia tu
utakuwa na uhakika wa kuvuna shilingi laki 3, na kwanini upate laki
tatu wakati unaweza kuongeza ukubwa wa ndoto yako ukapata zaidi ya laki
3? Ikumbukwe kwamba, wakati utakapokuwa unasubiri kuuza miche na pengine
kuipanda kwenye mashamba yako utakuwa unajishighulisha na kazi
nyinginezo kama bustani ya mboga nk.
Maadui wakubwa wa miti ni pamoja na magonjwa, wadudu, moto na wanyama
baada ya kuipanda. Adui mwingine wa kilimo cha miti ni mawazo yetu,
mawazo mgando yasiyotaka kuvumilia, ukipanda mti hasa ya mbao, nguzo nk,
usitegemee kuvuna baada ya mwaka mmoja, ni baada ya miaka 8 hadi kumi.
Kama utaona miaka 8 ni mingi usifanye hiki kilimo hakikufai. Tafuta
fursa nyingine.
Ikumbukwe kwamba, mafanikio yanatokana na mawazo au wazo la mafanikio.
Wazo linatengeneza fursa na kama utabuni wazo jipya kwenye mazingira
yako utaibuka kuwa mshindi.
Fursa za mafanikio zina gaharama yake, kuna
gharama ya muda, gharama ya pesa, na kama haupo tayari kulipia hizo
gharama hizo fursa zitakupita. Uchaguzi unabakia kuwa wako. “MY MOTTO IS GO BIG OR GO HOME”
Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta..!
MAWASILIANO. meshackmaganga@gmail.com
Sign up here with your email