Na: MROPE WA MROPE. Iringa.
Tena
maandiko yanasema, "yamtokayo mtu ndiyo yaliyoujaza moyo wake".
Wataalamu wa lugha kama Richards&Ogden walisema "kinachotamkwa
ni kiwakilishi cha picha iliyo kichwani mwa mtu".
Wataalamu
hawa waliungwa mkono na wataalamu wengine kama Edward Sapir na Nikolai
Trubetzokoiy ambao nao walinogesha kwa kusema "sauti inayosikika ni
kiwakilishi cha yale yaliyo kichwani mwa mtu na kichwani ndiko kuna
ukweli zaidi kuliko mdomoni". Hawa walienda mbali na kuweka mifano kama mtu akitamka "thelathini", "selasini" "thalathini", "thalathini" msikiaji atajua kinachomaanishwa ni 30 japo uhalisia wa maneno unakataa jambo linaloashiria kuwa kilicho kichwani mwa mtu ndicho hubeba maana halisi ya mtu. Ninachotaka kusema hapa ni kuwa kile utakachoilisha akili yako ndicho kitakachoujaza moyo wako na hatimaye matamshi yako.
Swali la kujiuliza
hapa, kitu gani unailisha akili yako? Stori na masimulizi yanayokujaza
uoga au maelezo yanayokupa ujasiri? Hayo yaliyojaa katika akili yako
ndiyo yanayokusukuma katika namna fulani ya kutenda.
Kama
leo unafuatilia fulani analea mtoto ambaye hajamzaa yeye maana yake
lazima uwe mtumwa wa kufuatilia hilo na likijaa kichwani mwako lazima
utafute pa kulitamkia ili nafsi yako iwe na amani.
Kifupi
hapo unakuwa umeajiriwa na umbea na utakuwa mtumwa wa huo umbea jambo
ambalo halina faida na maisha yako. Kama akili yako imejaa mambo
yasiyokuhusu utajikuta unasukumwa kutamka hayo yasiyokuhusu na watu
wakitaka mjadili yanayowahusu hasa hatima ya kimaisha utaona hayana
maana.
Nikuambie kuwa unahitaji sana umakini katika
mambo unayoingiza kichwani mwako maana ndiyo yanayojenga maisha yako.
Maisha yako yanaathiriwa na unachowaza na kutamka. Maisha yetu ni
uchaguzi juu ya mambo mawili tu yaani mazuri na mabaya. Wengi watasema
mimi huwa nachagua mazuri na si mabaya lakini yawezekana hayo ni mazuri
kwa mujibu wa uliyoyajaza kichwani mwako na wala sio uhalisia. Teja
anaona unga ni bora kuliko kuku, lakini je unga ni bora kuliko kuku? La
hasha lakini ni bora kwa mujibu wa yale aliyoyajaza katika kichwa chake.
Kwa mtindo huu wapo wengi sana katika maisha haya wanaochagua "unga"
(madawa ya kulevya) badala ya "kuku" na wanajiona wamefanya uchaguzi
sahihi katika maamuzi yao.
Unapokuja wakati wa maamuzi
ndio wakati wa kufanikiwa au kuharibikiwa, kupanda au kushuka, kujenga
au kubomoa na bahati mbaya muda wa maamuzi kila mtu hujiona yupo sawa
ila matokeo ya maamuzi ndiyo husema ukweli. Kwa hiyo niseme mapema kuwa
maamuzi yanatokana na kile tulichohifadhi katika store ya maamuzi na
kama stoo ya maamuzi imejaa mambo mabaya kwako yatakuwa mazuri tu kama
ilivyo kwa teja kuchagua unga.
Ninachotaka kusema ni
kuwa lazima uiheshimu sana akili yako na unachokipokea katika akili
yako. Tafuta maarifa ili uwe na machaguzi bora katika stoo yako ya
maamuzi.
Hapa hakuna kukwepa maana mafanikio ni matokeo
ya maamuzi na maamuzi ni matokeo ya uchaguzi wa yaliyo katika stoo ya
kichwa chako na kinachochaguliwa toka stoo ya kichwa chako ni matokeo ya
kile ulichokitafuta na kukiweka kichwani mwako. Wapi unatafuta mambo ya
kuingiza kichwani mwako ambayo ndiyo huamua maisha yako???
ALOYCE MROPE, Che Mrope Wa Mrope (fb), Mbeba Maono (fb page) 0766656626/0715366010/0787641417
Sign up here with your email