.

NAFASI YA MALENGO NA NDOTO KATIKA MAFANIKIO

    



Na: Meshack Maganga, Iringa.
Tangu nilipoandika makala yangu ya mwisho BINADAMU WOTE WENYE MAFANIKIO DUNIANI HAWACHOKI KUTAFUTA, sikupata muda wa kutosha kuandika makala nyingine hii ni kwa sababu ya shughuli za shamba na kazi nyingine za kijamii nilizonazo. Siku chache zilizopita nilikuwa kwenye mapumziko ya
siku 4, ilisafiri kutoka Iringa kwenda Sumbawanga,kabla ya safari ya sumbawanga  nilikuwa nimesafiri  kutoka Iringa kwenda Dar kwa ajili ya kununua vitabu, kuna duka maarufu sana pale mtaa wa Samora lijulikanalo kwa jina la ‘THE HOUSE OF WISDOM’ Nilinunua vitabu vingi lakini nitataja vichache hapa , Think Big cha Donald Trump, Advanced Selling cha Brian Tracy, The End of Poverty cha Jeffrey Sachs, The Millionaire Brain cha Donny, C. Na Winning The War against Poverty. Nilipomaliza kusoma kitabu cha Think big cha Trump na Winning The war against Poverty kwakweli nilijikuta nipo kwenye ulimwengu wa mafanikio kabisa, sikuona wingu la kushindwa mbele yangu.

Niliwahi kuandika kwamba, mafanikio ya kijamii na kiuchumi waliyonayo binadamu wenye mafanikio ni matokeo ya uwezo wao wa  kupanga na kufikiri na kuyaweka mawazo hayo kwenye vitendo. Na umaskini nao ni matokeo ya mawazo na mtazamo wa binadamu walioshindwa na wanaoendelea kushindwa kila kukicha.

Binadamu ndiye kiumbe cha pekee kinachotakiwa kubadilika kila siku kimwili, kiakili,kifikra,kiuchumi,kiutamaduni,kiroho  na hata kiuongozi wa  kwenye biashara yako.Ukitaka kuwa huru kiuchumi na kuondokana na unyonge wan a vifafa vya kiuchumi, jambo la kwanza ni kubadili mtazamo wako na kuongeza ufahamu wako kuhusu mafanikio.

Vitabu vya aina mbalimbali vya mafanikio na wataalaum wa mambo ya mafanikio na wajasiriamali kwa ujumla wao, wamekuwa wakisisitiza kwamba ili jambo lolote lifanyike na kujitokeza katika umbo lake la nje basi ujue hiyo ilikuwa ndoto ya mtu. 

Ukiona bodaboda imebeba abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine ujue hilo wazo la kutengeneza bodaboda ili itumike kwenye usafiri lilianza kama wazo kichwani mwa  huyo aliyebuni bodaboda.
Nimesoma makala ya mjasiriamali Joel Brown, iitwayo ‘10 Secrets on Successful Entrepreneurship’ aliyoitoa katika tovuti yake, anasema mafanikio yapo kwa ajili ya mtu yoyote  yule kuyachuma, lakini ili mtu afanikiwe lazima ajue au azingatie mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na washauri wake (Mentors) watu hao ni wale waliofanikiwa kwenye mambo anayoyafataka kuyafanya. Binafsi nilijifunza mambo mengi Sana kwa walezi wangu. Ninaanda makala isemayo ‘NILICHOJIFUNZA KWA MAMA YANGU KUHUSU UJASIRIAMALI’

Kila jambo lenye  mafanikio kilianza na ndoto. Unahitaji kuwa na njozi zako zilizo thabiti kama vile kuwa na biashara kubwa inayogusa maisha ya watu, kuwa  tajiri n.k. lakini mafanikio hayaishi katika ndoto tu, inabidi ufanye juhudi ya kubwa sana  – yaani kujenga taswira ya kile kitu unachotaka kukipata kwenye maisha yako. Mara ukishapata ndoto, basi mawazo yako yanatakiwa kujenga picha halisi ya jambo ulitakalo. Unatakiwa ujenge picha ya kitu utakacho, kana kwamba umeshakipata. Kila upatapo nafasi na  fursa jenga mawazo haya ya mafanikio kichwani kwako.

Kila mara mawazo ya kitu unachotaka kukipata yanapokujia, iwe mchana, usiku, asubuhi , jioni, wakati wowote ule, hata kama unakula. Unacheza upo kazini, hata unapokuwa umelala, mawazo yakija, amka yaweke sawa akilini mwako. Kwa mfano, itakuwaje nitakapoongeza fedha zangu mara mbili, itakuwaje nitakapofanikiwa kupata diploma au au digri yangu ? maisha yangu yatabadilika kiasi gani nitakapofanikiwa kupata mtoto?, Biashara yangu itakuwaje nitakapofanikiwa kuongeza .mtaji wangu hadi kufikia shilingi milioni kumi au ishirini n.k.

Mabingwa wa menejimenti wanafundisha umuhimu wa kutafakari kwa picha – yaani kuona mambo katika mawazo kama vile njozi imeshakamilika. Kwa mfano ukitaka kuwa tajiri hebu fikiria tayari unaishi katika nyumba ya kifahari yenyekilakitu cha anasa na wakati huo huo una akaunti benki iliyojaa fedha. Kitendo cha kujenga mawazo namna hii kinatakiwa kiwe cha kudumu. Kila saa unatakiwa kudikiria kwamba umeshafanikiwa (au utafanikiwa katika siku za karibuni) . mawazo kama haya yatakusukuma ili uongeze bidii zaidi katika kufikia malengo yako.

Siku zote nikiamka, nikiwa ofisini kwangu, nikiwa ninaendesha gari hajawahi tokea hata siku moja nikasahau kilimo cha miti, ninakipenda, kimenipa changamoto za maisha na kinanipa uhuru wa kiuchumi.Kama unaichukia kazi unayoifanya kamwe huwezi kufanikiwa hataukifanya katika miongo kadhaa. Unaweza kulazimisha kuifanya kazi Fulani hadi ukawa gwiji wa kazi hiyolikini lakini kamahupendi kazi hyo huwezi kupata mafanikio makubwa. 

Utaweza kufikia kiwango cha juu kabisa chautendaji nakufanya yale unayotakiwa kufanya kwa mafanikio makubwa kabisa endapo tu utafanya mambo yanayokufuhisha au mambo unayoyathamini sana.Wajasiriamali wanaofanikiwa  mara nyingi hujikuta wanatumia muda wa saa 15 au 18 kila siku bila kuchoka wala wao kujua, kwa sababu tu waipenda shughuli wanayoifanya.

Binadamu tumeumbwa tuwe na kiasi, na kama wewe unataka kuwa mwanadamu mwenye mafanikio hakikisha unafanya mambo machache kwa muda maalum. Inafaa kukubali ukweli, haiwezekani mtu akawa na uwezo wa kufanya kila kitu. Kila mmoja wetu anayo mambo anayoweza kufanya vizuri sana mengine anaweza kuyafanya kwa shida na yapo mambo ambayo hawezi kuyafanya kabisa. Kwa hiyo, ili uweze kufanikiwa, inakupasa kujichunguza ili kujua ni mambo gani unayoweza kuyafanya vizuri kabisa. Hayo ndiyo mambo yakuzingatia nakushikilia kwa bidii zote. Njia mojawapo ya kufanikiwa ni kuiga vitendo vya watu waliofanikiwa. Lakini hapa unatakiwa kuwa mwangalifu. Ni lazima umuige mtu Yule alefanikiwa. Lakini hapa unatakiwa kuwa mwangalifu. Ni lazima umuige mtu Yule aliyefanikiwa katika fani unazozimudu. Kwa mfano, kama rafiki yako amefanikiwa katika uchezaji wa mpira wa miguu hadi amekwenda Ulaya na anachezea timu ya Uingereza ya Manchester, basi si lazima uige anavyofanya hali ya kuwa wewe huna stadi za michezo. Kufany a hivyo, unapoteza nguvu zako bure. Kama kwena Ulaya ndiyo mafanikio, ni vizuri ujue kwamba Ulaya wanakwenda watu kwa sababu mbalimbali. Unaweza kupelekwa Ulaya na muziki, Ualimu, Udaktari n.k. wekeza nguvu zako katika fani ile unayoimudu barabara.

Ukiambiwa ama kusikia kwamba ulizaliwa ili ufanikiwe huo ni ukweli ni mpango wa Mungu uiishe maisha ya utele. Katika kitabu chake kiitwacho The Fountain, Any Rand, anasema , si kawaida ya binadamu wala kiumbe chochote kile kinachoanza shughuli yoyote ile kuanza kwa kukata tama. Tulizaliwa kufanikiwa na si kushindwa. Lakini bado uchgauzi utabakia kichwani kwako, kuwa mshindi au mshindwa, kumbuka kuwa  Ukiambatana na watanzania wenzako WATANO walioshindwa, na wanaoendelea kulalamika bila kuchukua vitendo na kufanya Kazi kwa bidii, basi wewe utakuwa Mtanzania namba SITA atakaye shindwa kwenye Nyanja zote za Maisha. Utafubaa badala ya kung'aa. Chagua watanzania wapiganaji na wapambanaji, jifunze kwao na kuna msemo wazamani usemao Eagles fly alone.

Ukiwa ama kama unataka kuwa mjasiriamali lengo lako  kubwa hapa litakuwa ni kuzibaini fursa na kujiamini kwamba ni haki yako kufanikiwa. Lazima uwe na imani kubwa sana na mipango yako, uwezo wako na uwe na imani na nafsi yako mwenyewe. Lazima ujenge  imani kubwa kwamba unaweza kubuni mipango mizuri na kasha ukaitekeleza. Kadri unavojenga imani juu ya malengo yako ndivyo hivyo utakavyoongeza nguvu na uwezo wa kutekeleza mipango hiyo . hata hivyo, unatakiwa kuwa jasiri pia, kwa kuwa tayari kutia mkono kizani, yaani, kufanya maamuzi juu ya mambo ambayo huna hakika nayo. 

Ndoto na malengo ni kama njia ndefu sana itahitaji muda na mikakati kukamilika, Tulipo kuwa tumeanzisha kampuni ya Fresh farm and Trading, tulipitia michakato na vikwazo vingi sana wakati ule tukiwa ndio tumetokea chuo, tulikutana na marafiki waliosema kila walichokiona, ilibidi kusafiri kila siku kilometa 89 kutoka Iringa mjini mpaka Mufindi yalipo mashamba yetu, tulitumia mpaka senti ya mwisho na ilifika muda tuakaanza kukopa, tuna mshukuru Mungu kwa vile ndoto na malengo yetu hayakufa, kwa sasa tupo kwenye hatua nzuri sana. 

Tukitaka kufanikisha ndoto zetu maishani, tuanze leo kutekeleza malengo yetu, tuwe na mipango mikubwa na midogo, tusikae kwenye makundi ya walalamikaji, kwa sababu hata ukilalamika san asana sana kichwa kitakuuma kwa sababu hakuna bianadamu aliyeumbwa ili ahangaikie ndoto zako, mwanadamu wa kwanza ataketimiza ndoto na malengo yako ni wewe.

 Itaendelea: Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta..!
MAWASILIANO.
meshackmaganga@gmail.com https://www.facebook.com/pages/Fresh-Farms-Trading
Previous
Next Post »