.

‘Kukurupuka’ kunavyorudisha nyuma wajasiriamali...!




Na: Meshack Maganga- Iringa.

Kwa muda mrefu sasa, Baadhi yetu tumekuwa tukitamani kufanya ujasirimali, na jamii yetu kwa mapana yake, tumeshaamini kwamba ujasiriamali unalipa, na mtu yeyote kwenye jamii yetu anae fanya ujasiriamali anaonekana kwamba ni mtu mwenye pesa. Hata kama
ameenza jana. Tunasahau kuchunguza sababu zilizo msukuma huyo mtu kuanza ujasiriamali, tunasahau shida na changamoto alizozipitia huyo mtu katika safari yake ya ujasiriamali.
Kimsingi, ujasiriamali Tanzania umeshika kasi miaka ya 2000, hasa kutokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kuruhusu  uwekezaji na ndipo msamiati wa Ujasiriamali uliposhika kasi na kuboreshwa na sera na sheria mbalimbali za uchumi
Kutokana na hali hii, tumeshuhudia watu wengi wakijitoa kimasomaso kuanzisha biashara au kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali. Niwahi kusoma makala moja siku za nyuma kwamba, David McClelland ambaye ni mwanasaikolojia kutoka chuo kikuu cha Havard nchini Marekani aligundua tabia za kisaikolojia zinazojengeka ndani ya mjasiriamali ambaye amefanikiwa kibiashara. Akifafanua hoja yake msaikolojia huyo alisema, wajasiriamali waliofanikiwa huwa na hamasa, malengo na huwa tayari kutumia muda wao kufanya kile anacho kitaka.
Inasemekena kwamba msamiati huu ulianza kutumiwa kwa mara ya kwanza na mwana uchumi maarufu Richard Cantillon wa Ufaransa mwaka 1755 na baadaye ulipata mashiko kuanzia miaka ya 1800 ambapo wafanya biashara wenye mitaji mikubwa “mechants” kutoka  Ulaya walipoanza kuzunguka dunia  wakitafuta malighafi na madini kwa ajili ya viwanda vyao binafsi na vile vya makampuni yao.
Katika makala hii, tutaangalia ni kwanini watu wengi wamekuwa hawafikii malengo yao wanapoingia kwenye ujasiliamali na biashara nyingine ndogondogo.(Small business owner)  Nitaelezea kwa kifupi sababu niliziziona mimi binafsi.
Kwakuwa Ujasiriamali umeonekama kuwa muarobaini wa kuondoa umaskini na kutatua tatizo la ajira, watu wengi hasa vijana wanaotoka vyuoni, na wastafu  wamejitokeza kwa wingi sana kufanya ujasiriamali na hasa upande wa kilimo. Sababu chache nilizoziona mimi na zinazo changia wajasiriamali hao kuendelea kulalamika, ni hizi zifuatazo:-
Kukosa malengo madhubuti na madhumuni ama dira ama kuwa na  sababu  moja hasa ya kutaka pesa .  Tumekuwa watu wa kukulupukia mambo tumekuwa tukisikia  kwamba biashara fulani inalipa basi wote tunakimbilia kufanya hiyo biashara. Miaka michache iliyopita nilipokuwa mwanafunzi wa chuo, kulizuka kampuni moja iliyohamasisha wateja wake kuweka pesa zao kwa muda na baada ya muda wateja hao wengepata kiasi kikubwa cha pesa ‘kuvuna’. Wengi walioingia kwenye mtego huo bila kufanya utafiti wala kujiuliza. Baada ya muda mfupi kampuni ile ilipotea na walioingia na kupeleka pesa zao kwa mtindo wa ‘ kukulupuka’ waliishia kulia na kulalamika. Kimsingi, ili ufanikiwe kwenye ujasiriamali, ni lazima uwe na lengo, malengo yaliyo simama,malengo yanayopimika tena yenye muda maalumu, malengo yatakayo gusa maisha yako na yanayogusa jamii inayokuzunguka.
     Kutokuwa na njaa ama kukosa hamasa ya kutafuta maarifa siku zote. Hii ndio ajabu kubwa niliyoiona. Mtu anataka kufuga kuku, na anaamini kwamba akifuga kuku, atapata faida kubwa baada ya mika michache. Mtu huyohuyo anatamani kupata pesa inayo tokana na kuku atakao wafuga, akiambiwa aende kwenye semina za kufuga kuku hataki kwenda kwenye semenina hizo. Anapewa vipeperushi ama vitabu vya ufugaji wa kuku anaona uvivu kusoma, anataka asomewe. (Unafikiri kuna mtu aliiumbwa ili ahangaikie ndoto na malengo yako? Go big or go home). Mwingine amesikia kwamba kilimo cha vitunguu kinalipa, bila kufanya utafiti kwa kusoma ama kuwatembelea walima vitunguu huko mashambani na yeye ananza kulima, hajasoma, hajafanya chochote, ana kukulupuka tu. Yani mtu anaanza kufanya jambo bila kujua na kufahamu misingi ya jambo hilo. Mtu anaanza kulima vitunguu, hafahamu hata aina ya mbegu, hafahamu atapata soko wapi baada ya kuvuna, hafahamu kitalu ni nini, madawa, kanuni za umwagiliaji nk, hajawahi kuyaona mashamba ya vitunguu, zaidi ya kukiona kitunguu kwenye mboga. Mtu huyo hawezi kufikia malengo yake. Akipata hasara anaelekeza lawama kwa mtu aliyempatia tarifa ya aina ya ujasiriamali anaofanya.

Kutojiamini, Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza. ukitaka kufanikiwa katika jambo lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza. Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini.  Inatokea mtu anataka kufanya jambo fulani, lakini moyo wake na ndani ya kili yake kuna hofu kubwa imetanda. Hofu ya kushindwa, hofu ya kuchekwa, hofu ya kupoteza pesa, hofu kuogopa maneno ya jirani zake. Kuna wanaogopa kuitwa majini kama vile ‘muuza samaki’,  ‘mfuga kuku’, ‘muuza mashati’, ‘muuza mahindi ya kuchoma’, ‘mlima vitunguu’, ‘muuza karanga’ nk. Ukiwa na hofu kama hii, huwezi fika mbali na maana yake ni kwamba umekulupuka tu, ama umesukumwa na changamoto za kijamii ndio maana ukaingia kwenye hilo jambo.  Nilipokuwa nimeanza kilimo cha miti huko Mufindi, sikuogopa kuiitwa ‘mlima miti’, hii ni kwa sababu malengo yangu na mawazo yangu ya kina hayahusiani wala kufungamana na binadamu yeyote yule hapa duniani, mimi ni mimi na wao ni wao.

Uvivu uliopitiliza ama kutokuwa watendaji na waongeaji sana. Wapo walioamua kuruhusu mitandao ya kijamii na michezo ya kuigiza kwenye televisheni kutawala mawazo na akili zao, wakiwa mitandaoni wakisoma jambo la kibiashara wanakulupuka kulifanya. Tofauti na kwenye ajira ambako unaweza kutumia maneno ya uongo ukachelewa kazini kwa siku moja ama masaa na mshahara wako ukawa palepale. Katika maisha ya kijasiriamali  ni kusonga mbele na si kupanga peke yake. Ama kuwa na lundo la makaratasi yasiyo fanyiwa kazi. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno ishi matendo. Kuna kipindi utalazimika kupunguza muda wako wa kulala na kuwahi kuamka ili utekeleze ndoto zako.

     Kukata tamaa, ni vizuri kabla ya kuanza ujasiriamali, ujipe muda wa kutafakari, usiingie kufanya ujasiriamali kisha baada ya muda ukapotezwa na upepo na maneno ya walioshindwa. Kukatishwa tamaa, husababishwa na mambo madogomadogo. Kama vile ndugu, watakao kupatia ushauri wa bure, kusikiliza maneno ya mitaani na kusikiliza matukio ya kijamii ama kujiingiza kwenye harakati ambazo hazina tija kwenye maisha yako nk. Ukiona mtu ameanza ujasiriamali na baada ya mwaka akaacha  ama kukulupukia jamabo jingine, wakati kuna binadamu wengine bado wanapambana  basi lazima anakuwa kwenye kundi la wanakulupukia mambo, na takuwa kwenye kundi la Wanadamu wanaondesha na matukio ya kijamii.

 Kukosa msimamo, na kuruhusu kichwa chako kupokea kila aina ushauri. wengi wetu tumekuwa watu wa kufanya kila jambo.  Kuna wanaofuata bendera fuata upepo, hawana misimamo. Mtu huyohuyo anataka kufanya biashara ya bodaboda, anataka kufanya biashara ya daladala.Mtu yuleyule anataka kulima vitunguu, auze chips, afungue duka la nguo,  kisha anataka kufuga samaki, afuge kuku,auze vocha kisha aanzishe mgahawa,tena kwa wakati mmoja bila kujipa muda.  Mjasiriamali aliyeamua kupata kitu fulani maishani hajui sababu za kushindwa na wala hana sababu zinazoweza kumzuia.



Ninapohitimisha makala hii fupi, ifahamike wazi kwamba,  kwa vile watanzania hatuna utamaduni mahususi wa kujisomea makala na vitabu  vya utambuzi na maarifa, tutaendelea kukulupukia mambo na mwisho wake tutajikuta tumekosa yote, muda,  pesa, na tutajikuta hatuna uhuru wa kujiamulia mambo yetu binafsi. Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu asiyekuwa na msimamo, binadamu anae kukulupika mambo kabla ya kutafakari,  mwanadamu anaeruhusu kichwa chake kupokea mazagazaga yasiyokuwa na tija, lakini pia dunia hii ina upande mwingine wa mafanikio. wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, na wanajua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe. Uchaguzi unabakia kuwa wako.
“MY MOTTO IS GO BIG OR GO HOME”Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta..!MAWASILIANO. meshackmaganga@gmail.com
https://www.facebook.com/pages/Fresh-Farms-Trading



















Meshack Maganga 2014
Previous
Next Post »