.

Salamu za mwaka mpya kutoka ‘FRESH FARM & Trading’---2015.


                       

    ‘Usiishi maisha yale yale yasiyo badilika, wewe siyo Jiwe’.



Na: Meshack Maganga -Iringa.

Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote aliyotutendea mwaka uliopita wa 2014. Tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kutulinda Watanzania kama Taifa lenye mshikamano wa hali ya juu sana, na zaidi kwa kutupatia fursa za kila aina.

Mwaka uliopita ulikuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa sana kwetu,kuanzia kiroho, kijamii na kiuchumi. Tumeendelea kufanya vizuri kwenye kilimo.Mwaka wa 2014, tulijikita zaidi katika kujifunza kilimo cha miti na mbegu bora.Tulitembelea kituo cha Tanzania Tree Seeds Agency kilichopo Iringa mjini na kujifunza juu ya upandaji miti ya nguzo na mbao. Na sisi tulirudi mashambani kwetu na kuwashirikisha wakulima wenzetu yale tuliyojifunza. Tulipopata muda wa kutosha tuliandika kwenye mitandao ya kijamii na
waliopenda waliwasiliana na sisi na kuja kujifunza.
Mwaka huo pia,tulijifunza ufugaji wa samaki, na kuanzisha mabwawa machache kwa kutumia mtaji mdogo sana na ambao kila mwenye uchungu na maisha yake anaweza kuufanya. Zaidi ya hayo, tulijikita kwenye kilimo cha mbogamboga kama matango, vitunguu na pilipili hoho. Ni moja ya kazi anazoweza kuzifanya binadamu yeyote akipenda. Na hasa anaefahamu sababu yay eye kuwepo duniani.
 Tumeuanza mwaka mpya wa 2015 ambao ni mwaka wa kufanikiwa sana kiroho, kimwili na kijamii. Na Rai yangu kwa watanzania wenzangu ni: ­- 

Moja, weka malengo, yaandike na uyafanyie kazi, hii ni kwa sababu, mwisho mzuri katika maisha yako, hautatokana na vyeti ulivyopewa na kukusanya ulipokuwa shuleni na chuo. Bali hatua unazochukua katika kutekeleza malengo yako. Tafuta washauri. Kaa na marafiki wazuri na uige mazuri wanayofanya.  Wewe ni Nuru na chanzo cha mafanikio yako popote pale ulipo . Giza la kushindwa na kulalamika unaloliona linatokea wapi? kumbuka wewe ni wewe.  Nilipokuwa nimeanza kilimo cha miti huko Mufindi, sikuogopa kuitwa "Mlima miti" hii ni kwasababu mawazo yangu ya kina na malengo yangu, hayafungamani na Binadamu yoyote hapa duniani. Mimi ni Mimi na wao ni wao. Msomaji unayo ruhusa ya kuipinga ama kuikubali falsafa yangu.

Mbili, fanya kazi uzipendazo na zaidi ufanye miradi mingi ya kutosha, mwaka uliopita mwezi wa 11, nilibahatika kuonana na Mwana mama mpambanaji sana Haika Lawere. Nilikuwa nimemwandikia email siku nyingi kuomba muda ili nijifunze kwake. Kwenye mazungumzo yale nilijifunza sana na moja ya sentensi alizoniambia ni "Usitegemee chanzo Kimoja cha mapato, (utafulia na sikuzote utakuwa ni binadamu wa kulalamika) kama wewe ni mfuga Ng'ombe fuga watatu ili mmoja akifa ama kuugua upate maziwa kwa mwingine." Ninakubaliana na Haika, hasa ukizingatia kwamba, ukitegemea kuuza muda kwenye ajira yako na mwisho wa mwezi upate malipo yaitwayo mshahara pekee kuendeshea maisha, lazima utapata kifafa cha kiuchumi. 

 Niliwahi kuandika kwamba: “Tabia na mawazo yetu ndiyo adui zetu wakubwa katika kufikia ndoto zetu." Kuna tunaotamani kufanikiwa lakini kufanya kazi zitakazo tufanikisha hatutaki...(uvivu). Kuna tunaotamani kufanikiwa lakini kwenye mawazo yetu ya kina kumejaa wasisi na kutojiamini. Tupo tunaotamani kufika mbali sana kiuchumi, kimwili na Kiroho lakini bado mawazo yetu hayaendani na imani zetu kuhusu mafanikio, mtu anataka afanye jambo leo (wanaita now now) jumatatu na kesho jumanne awe amefanikiwa.Tunatakiwa kujaza picha na kauli za mafanikio kwenye mawazo yetu. Mafanikio hayachagui mtu kwa kuangalia mkoa anakotoka wala rundo la vyeti alivyopewa chuo, jinsia wala umri. Fanikio la awali la binadamu ni kuamini katika mafanikio. Na wahenga walisema “Adui wa mtu ni mtu mwenyewe". Na uchaguzi unabakia mikononi mwako, kuamini kwamba utafanikiwa ama kuamini kwamba hutafanikiwa...!

Kwa wale watakao amua kuwa wakulima na wajasiriamali kwa ujumla, watalazimika kufanya chaguzi Mbili mhimu: 1. Kufanya kazi kwa bidii ili ufanikiwe na 2. Kulala sana na kuendelea kulalamikia ugumu wa maisha na uendelee kubakia pale pale. Kwenye ujasiriamali utalazimika kufanya kazi mhimu mwenyewe kwa nguvu zako na kwa masaa mengi zaidi, utalazimika kusimamia kazi zako mwenyewe hata kama una wafanyakazi wako, na iwapo utajidanganya kutelekeza kazi zako kwa vibarua wako “utafulia". Na ukiona kwamba huwezi kufanya kazi masaa mengi kwa kutamani "kujiachia" huko mtaani, ni bora uachane na ujasiriamali ama kilimo na uingie mtaani kusaka ajira ili upate muda wa kuzunguka kwenye viti vya ofisini. 

Kuna walioamini na kuendelea kuaminishwa kwamba vyeti vya madarasani vitawakomboa kiuchumi. Kama bado una mawazo ya kizazi cha ‘Wakati wa viwanda- Industrial Age’ badilisha mawazo yako. Nilipokuwa chuo kikuu, nilidhani kuwa elimu yangu niliyoipata itakuwa ni jawabu tosha katika shule ya maisha. Kumbe sikuujua ukweli. Unaweza kukimbia shule za madarasani lakini huwezi kukimbia shule za mtaani.

 Kabla sijamalizia makala hii ningependa kurudia maneno yangu niliyoyandika juzi kwenye ukurasa wangu wa ‘face book’ kwamba, Kauli za ‘Kupata ni majaliwa’ Ng’ombe wa maskini hazai’ serkali haituthamini’, ‘sijasoma’, mimi ni mlalahoi/ mlalatabani, 'mkoa wangu ni wa pembezoni, kabila letu limesahaulika, nk, ni kauli za kimaskini, ni kauli za kutafuta visingizio. Tumia vizuri mawazo yako ya kina ufanikiwe. Jielimishe, soma vitabu vingi vya mafanikio, anzisha biashara ndogo upendayo ili iwekubwa, amua kufanya kilimo biashara, lima nyanyachungu, bamia, uza chapati, uza maji, fuga samaki, uza vocha, uza ugali, nk, amua kubakia palepale ulipo ukimsingizia shetani na wachawi, ama kuendelea kuwalalamikia viongozi wako wa kisiasa na kidini kwamba ndio chanzo cha ‘kufulia’ kwako, ama kuamua ‘kujitafuta’ na kuangalia ukuu wa Mungu ndani yako. Pigania kile ukitakacho usivunjwe moyo na waliochoka kiakili, waliochoka kufikiri, na wasiokuwa na malengo. Na wanaosema ponda mali kufa kwajwa.
“MY MOTTO IS GO BIG OR GO HOME”Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta..! MAWASILIANO. meshackmaganga@gmail.com. https://www.facebook.com/pages/Fresh-Farms-Trading

Meshack Maganga 2014
Previous
Next Post »