.

Nguvu Ya Ushirikiano Katika Ujasiriamali....



Na: Meshack Maganga, Iringa MERO investment GO BIG
Sasa hivi kutokana na ugumu wa masharti yanayowezesha watu kupata mahitaji kwa mikopo au njia nyingine, kuna idadi kubwa ya watu ambao wameamua kuazisha biashara kwa kushirikiana. Pengine wengine wamelazimishwa na ushindani uliopo kufanya biashara kama timu kuliko mtu mmoja mmoja.Lakini kama wasemavyo wataalamu wa mafanikio, mtu mmojammoja huwa anajikiza mwenyewe wakati mwingine.
Kama ni hivyo,watu wanapo kuwa zaidi ya mmoja, hata wawili,  ni suala lisiloweza kuepukwa. Hii haina maana kwamba, ushirika wa kibiashara ni mbaya, hapana. Bali suala ni kwamba uangalifu ni muhimu sana.
Ndoa inaweza kulinganishwa na mtu na mshirika wake kibiashara, kwa sababu ya kufanana mambo mengi, kati ya ndoa na ushirikiano wa kibiashara. “Hadi kifo kije kitutenganishe”  hiki ni kibwagizo cha kawaida kusemwa mbele ya kasisi kama kiapo kwa mke au mume mtarajiwa. Lakini ukifanya hivyo kwa mshirika wako kibiashara utakuwa hujaona mbali tena ni jambo la hatari sana.
Hicho tu ndicho kipengele ambacho ndoa na ushirikiano kibiashara vinatofautiana. Lakini maeneo mengine yote ni kama sawa.Ndoa imara na bora ni ile ambayo wahusika walijuana vema na kupanga mambo yote muhimu mapema. Walikubaliana au kupingana kuhusa watoto, kazi, wazazi na ndugu, imani na mengine. Walitafuta ufumbuzi wa kila kikwanzo cha baadaye kwanza.
Mara nyingi watu wanaoanzisha biashara ya (SOMA ZAIDI
  kushirikiana (partnership) huruka hatua moja muhimu sana: kuweka makubaliano kwa maandishi chini ya mwanasheria. Hata Kama utafanikiwa kuanzisha biashara nzuri na yenye mafanikio na mshiriki wako wa kibiashara, je, una mawazo kwamba mtakuwa pamoja katika biashara hiyo katika maisha yenu yote?
Biashara ambazo hazijitenganishi na wamiliki usalama wake ni mdogo, ukuaji wake ni wa kusuasua na urefu wa uhai wake daima huwa mashakani. Ingawa mimi nilikuja kugundua kuwa ‘kumbe’ nilifisika kwa sababu ya biashara zangu kukosa mfumo rasmi wa kiutawala, baadae nilipata funzo kubwa sana kuhusu hatua za uanzishaji na uendeshaji wa biashara katika mfumo wa kikampuni.
Wajasiriamali wanapofikia uamuzi wa kuanzisha kampuni (partnership) kuna hatua chache tu za kufuata. Kwanza wanatakiwa kuandaa nyaraka za kampuni, ambazo zinaeleza muundo na mfumo wa kampuni inayokusudiwa. Nayaraka hizi zinajulikana Kama, ‘Article of Association’ inaelezea muundo wa ndani wa kampuni wakati nyaraka nyingine ni ‘Memorundum of Association’ hii ikiwa inaeleza uwezo na mipaka itakayokuwa nayo kampuni inayokwenda kuundwa.

Hebu fikiria,umefikia umri wa miaka 90-bado kweli   utakuwa una uwezo wa kuchapa kazi katika ushirikiano  huo? Utafika muda,mtalazimika kuvunja ushirikiano wenu bila kujali kwamba mnapata faida au hasara. Kwa kuzingatia hili, anza ushirikiano na mshiriki wa kibiashara wako mkiwa na malengo. Mkifanya hivi pale pale mnapoanza ushirikiano wenu, mtavuna matunda yaliyo bora sana kwenye ushirikiano huo.
Kufanya biashara na mshiriki wa kibiashara ni sawa na janga linalosubiriwa kutokea. Olabisi na Saley walikuwa madaktari, kila mmoja alikuwa akifanya kazi yake Tanzania. Waliamua kwenda kuazisha hospital Namibia.Walipomuona mwanasheria kwa ushauri, aliwaambia wafanye makubaliano kimaandishi.
Katika kuandika makubaliano, Olabisi  alipinga mambo ambayo Saley alikuwa anataka yawemo katika mkataba huo. Baada ya miezi miwili ya majadiliano ya mkataba ule, Olabisi  alitoka kwenye chumba cha mwanasheria kwa hasira kutokana na kikao kuwa cha moto.Sasa huu ni mvutano uliotokea hata kabla ya ushirikiano wenyewe haujaanza.
Je,wangekuwa wameshaanza ingekuwa rahisi kwa tatizo hili kutafuti waufumbuzi? Olabisi na Saley  hawa kuongea tena ingawa walikuwa katika fani moja. Usije ukadhani kwa sababu tu, lengo letu ni kufanya shughuli fulani, kila kitu mnakubaliana. Ni vema, yote yakawekwa wazi, Hata yale yanayoonekana madogo kabisa. Watu wanaojiingiza katika ushirika wa kibiashara huku wakiwa na malengo ya muda mrefu ambayo ni malengo tofauti kabisa. Tengenezeni malengo ya muda ya mrefu kwanza, na yale ya muda mfupi yatokane na yale ya muda mrefu.
Peterson na Chrislouw walianzisha Kampuni yao wakiwa na kila mmoja hisa sawa na mwingine, yaani 50 kwa 50. Hii ina maana ya watu walio sawa, yaani kwa umiliki wa kampuni yao. Walianza biashara yao bila malengo yoyote,yaani kama walikuwa wanabahatisha ilikuwa ni aina ya upotezaji muda.
Mambo yakageuka na biashara yao kuwa kubwa na yenye mafanikio makubwa. Biashara yao ilivyozidi kuwa kubwa ndivyo uadui kati yao ulivyozidi kuwa wazi. Kuna wakati fedha inaweza kuwa ndiyo kigezo cha hisia zetu –ikiwa nyingi tunakuwa wakorofi, ikiwa kidogo tunakuwa wapole,au kinyume chake.
Ilitokea siku moja Peterson akilalama kwamba Chrislouw anatamaa na anenda kinyume na malengo yetu ya zamani kwamba tutawajali wateja wetu kwa kuzalisha bidhaa bora na kwamba Sasa hivi kitu muhimu kwake ni kutaka kuwa rais wa kampuni hii kubwa na kupata mamilioni ya fedha.
Peterson kwa upande wake, hakutaka kufanya kazi kwa bidii wala kuhitaji kuwa tajiri mkubwa. Alikuwa akihitaji kile ambacho kingeweza kuihudumia familia yake. Chrislouw kwa upande mwingine alikuwa ameachana na mkewe akiwa na watoto kadhaa –kazi yake ilikuwa ndio maisha yake.

Chrislouw alilalamika; Peterson anairudisha kampuni hii nyuma.Hufanya kazi kwa lengo la kuikuza kibiashara. Palepale mwanzo yangejitokeza haya yanayojitokeza sasa wakati wanajadili malengo ya muda mrefu. Kila mtu angekuwa ameonesha wazi ni kitu gani kinamvuta katika kuingia katika ushirikiano huo.
Kuondoa tofauti hizi kubwa walitakiwa wakati wanafanya makubaliano kuweka vipengele ambavyo vingemfanya Chrislouw aweze kununua hisa za Peterson Au makubaliano hayo yangekuwa yameainisha kwamba mshiriki wa kibiashara wa tatu angeruhusiwa kuingizwa ili kumpunguzia mzigo Chrislouw  wateja wateja wanapo kuwa wengi.
Lakini badala ya makubaliano kuwa 50/50 yangebadilishwa na kuwa labda sitini kwa arobaini ili kufidia kazi nyingi ambazo Chrislouw anafanya zaidi kuliko Peterson. Muda muafaka wa kuyaweka hayo yote ilikuwa ni pale mwanzoni wakati bado walikuwa na maelewano ya kirafiki, siyo ya kibiashara.
Ingawa mijadala ya kutengeneza makubaliano inakuwa na misuguano mikubwa, baada majadiliano, ushirikiano wenu utakuwa katika msingi imara.Badala ya kupotaza muda mwingi kwa ajili ya kutatua matatizo yatokanayo na kutofanya mabadiliko mapema, muda huo utakuwa ukitumika kwa ajili ya tija.
Biashara yeyote inaratibiwa na mazingira mbalimbali ya kisheria. Moja wapo ni kutakiwa kupafanya mahali pa kazi kuwa salama kwa wafanyakazi pamoja na kuwalipa stahili zao kwa wakati. Biashara yeyote ukiona haithamini wafanyakazi, watendaji ama vibarua wake basi uwe na uhakika kuwa anguko lake lipo karibu.
Tofauti na kwenye siasa ambako kipimo cha uzuri wa chama cha siasa ni wakati wa uchaguzi; kwenye biashara alama ya kwanza ya biashara ama kampuni kupoteza dira ni kukimbiwa na wafanyakazi, kupungua kwa wateja na kushuka kwa mauzo. Katika eneo hili kuna jingine ambalo ni kutoa bidhaa na huduma salama.
 Nilieleza kwa kina baadhi ya mambo ya muhimu yanayopaswa kuzingatia kabla na wakati wa kuanzisha biashara za ushirikiano (kampuni, patnashipu n.k). Wasomaji wengi wamewasiliana nami wakinipongeza na kutoa maoni yanayopanua mjadala huu. Leo ninaendelea na sehemu ya pili ya makala hii katika pembe zingine mtambuka.

Wengi wetu tumesikia watu waliokuwa marafiki katika biashara wakikorofishana. Kwa sehemu kubwa hii ina tokana na kufanya mambo kienyeji. Mike ni mmoja wa watu walikumbwa na matatizo kama haya: ‘mshirika wangu katika biashara aliamua kuuza biashara yetu bila ridhaa yangu.

Tulianzisha biashara yetu toka ziro hadi mauzo kufikia shilingi milioni mia sita Kwa mwaka anasema Mike. Halafu anaendelea, Nilikuwa ninachapa kazi kama punda na hatukuwahi kugombana. Lakini nyuma ya pazia, kwa kuwa hisa zake katika biashara zake katika biashara yetu ilikuwa asilimia 60 akawa amempata mnunuaji na kuamua kuiuza biashara yetu.

Alinilazimisha tuiuze; nilikuwa sina fedha za kununua hisa zake baada ya kuuzwa marafiki zangu wakaniona nina bahati baada ya kupata fedha nyingi. Lakini nilikuwa sijali sana kuhusu fedha. Nilimpoteza rafiki yangu mpendwa na kazi yangu niliyokuwa naipenda sana. Usaliti huu ulinishitua sana. Masalia ya mshituko huo bado yapo na ndio yanaisha kidogokidogo.
Yote haya ni matokeo ya kudhani mshirika wako anafikiri na kuamini katika kile unachoamini. Kuweka mambo wazi na kwa makubaliano kabla ya biashara ni muhimu sana. Fedha hubadili mitazamo ya watu, hasa wanaoamini kwamba, fedha ni kila kitu na wale wanao amini kwamba bila mtaji huwezi kuanza biashara.

Kwanza inabidi kufahamu kuwa hakuna watu waliozaliwa kuwa marafiki bora ama marafiki wabaya kibiashara. Watu wote wanatengenezwa kutegemea na mazingira ya kazi. Kwa maana hii si ndugu, mke wako ama familia yako watakaokuwa wasaidizi bora katika biashara zako.

Isipokuwa unatakiwa kuwa na mbinu sahihi za namna ya kuwapata watu makini watakaobeba uchungu kama ulionao wewe katika biashara zako. Kwa maana hii iwe ni watu unaohusiana nao kiundugu ama usiohusiana nao, wote unatakiwa kuwaajiri ama kufanya nao kazi kwa werevu mwingi.

Suala la kuwapata washirika makini linatakiwa kuanza na wewe kubaini tabia ama hulka za watu ambao utaendana nao katika mawazo na maamuzi ya kibiashara. Jambo la pili ni kuangalia matakwa yao ya ndani (motives) na la mwisho ni uwezo wako wa kuwajengea uwezo wa kufanya kazi na kukaa nao kwa muda muafaka.

Mjasiriamali maarufu duniani Robert Kiyosaki ambaye mwaka huu ameibuka kuwa mshindi wa Tuzo ya “12 days of Finance Winner” katika makala ya  "The benefits of being in Rich Dad's Business Owner Quadrant™ vs. Self Employed Cash flow Quadrant™ " ameeleza kuwa wakati alipokuwa akifanya biashara kwa kutegemea nguvu zake mwenyewe  na ujanja wake alioupata chuo kwa kupewa kazi binafsi ama za vikundi maarufu kama (individual assignment  or group assignment) na Profesa wake ama mhadhiri alijua atafanikiwa mapema baadaye kutokana na mabadiliko ya dunia akagundua kwamba kufanya biashara bila ushirika na wenzako ni sawa na ‘kutaka kuvuka bahari ya Hindi kwa Mtumbwi uliotoba’    

UJASIRIAMALI bila kuwa na mfumo rasmi wa uendeshaji ninaweza kuufananisha na ile hulka ya ndege aina ya mbuni ya kujificha mchangani. Mbuni kwa kawaida huwa ana asili ya kuficha kichwa chake mchangani pindi aonapo hatari ama anapotaka kuwa salama katika eneo lolote lile”.
Albert anasisitiza kuwa wajasiriamali wanapokuwa wamesajili rasmi (kampuni) au biashara zao, wanalazimika kuwa na mfumo rasmi wa kiutawala pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za kimahesabu. Kunapokuwepo na kampuni hailazimiki wamiliki wa kampuni wawepo ili biashara ziende.
Hii ni faida tofauti na ilivyo kwa wafanyabiashara binafsi (sole proprietor) ambapo wao ni biashara na biashara ni wao. Wao wakifa na biashara zinawafuata nyuma yao makaburini. Lakini wamiliki wa kampuni wakifa, ama mmoja wao akifariki kampuni inaendelea kuishi kwa kuwa yenyewe ni mtu kamili kisheria (legal person) na haki ya kila mmoja itakuwepo kwasababu kuna Legal Document.
Kwenye makala ya "South Park's" Investing Lesson: Imeelezwa kwamba, wenye ndoto ya kuanzisha biashara ya kushirikiana wanatakiwa kuwa na Mpango wa biashara (Business Plan) Mimi ni mmoja wa wenye ndoto hiyo (partnership).
Mpango biashara, ambao kwa maana ya kawaida (surface meaning) na maana ambayo mwalimu wangu wa chuo kikuu Dr.Mahali aliwahi kuiniambia “ni vifaa vya kufanyia uamuzi wa kibiashara”. Kwa kiasi fulani, muundo na yaliyomo kwenye mpango wa biashara hutokana na malengo ya pamoja ya washiriki. Ni sharti mpango wa biashara ijumuishe kila habari inayohitajika kuamua kutekeleza lengo fulani la kibiashara.
Kwa mfano, mpango wa biashara wa shirika lisilo la kifaida hufafanua ukubalifu kati ya mpango wa biashara na malengo ya shirika hilo. Kimsingi washiriki wa mtaji hujihusisha na uwekezaji wa awali, uwezekano wa kufaulu na kutathimini jinsi ya kutamatisha. Mpango wa biashara wa mradi unaohitaji fedha utahitaji kueleza kwa nini rasilimali zilizopo kwa sasa, nafasi za biashara zinazoibuka, na faida ya ushindani endelevu itawaletea ufanisi mwishoni.
Utayarishaji wa mpango wa biashara huhitaji maarifa kutoka kwa taaluma za biashara mbalimbali: fedha, na usimamizi wa wafanyakazi, usimamizi wa ujuzi-nafsi, usimamizi wa ugavi, usimamizi wa shughuli, na masoko, miongoni mwa mengine. Ni jambo muhimu kuangalia mpango wa biashara kama mkusanyiko wa mipango midogo midogo, moja kwa kila taaluma kuu ya biashara.
Mpango wa biashara mzuri unaweza kusaidia kufanya biashara nzuri iwe ya kuaminika, ya kueleweka, na kuvutia kwa mtu ambaye hana ufahamu wa biashara hiyo. Uandishi mpango mzuri wa biashara haumaanishi kuwa utafaulu lakini unaweza kusaidia katika kupunguza uwezekano wa kutofanikiwa kwa biashara ya ushirika.
Nilipotembelea nchi ya Zambia miaka miwili iliyopita nilibahatika kusoma magazeti na vitabu mbalimbali lakini moja ya makala ambayo iliniingia kichwani  kama mjasiriamali na mpenda biashara ya ushirikiano, na nimhimu kunukuu katika Somo la  leo ni ile ya Rais wa kampuni ya ‘Colgate’ duniani  Ian Cook. Yenye kichwa kisemacho   Kanuni na maadili mema ya Colgate-palmolive.
Ian Cook anasema kuwa Uamuzi wako ni moja wapo ya mali yako ya thamani sana. Unafaa kuepuka shughuli ama ushirika wowote ambao unagongana na ama unaonekena kugongana na uwezo wako wa kufanya uamuzi wa kujitegemea kwa masilahi ya Kampuni. Migongano inaweza kutokana na hali nyingi. Ni vigumu kuelezea yote hapa, na haitakuwa kila mara rahisi kutofautisha kati ya shughuli kamili na zisizo kamili.
Katika makala hiyo washirika wa kibiashara wanasisitizwa kwamba, unapokuwa na hoja amadukuduku, muone meneja wako ama mshauri wako wa kitengo cha sheria kabla ya kuchukua hatua yoyote. Miongozo ifuatayo inatumika katika hali ya kawaida ya migongano. Usifanye uwekezaji wowote unaoweza kuathiri uamuzi wako wa kibiashara.
Sera za Kampuni zinakataza watu wa Colgate kumiliki hisa ama kuwa na hamu ya kumiliki katika Kampuni inayoshinda na ama inayofanya biashara na Colgate. Kizuizi hiki hakitumiki kwa kumiliki viwango vidogo (kwa ujumla chini ya 1%) vya hisa za Kampuni inayouza hisa kwa umma ila tu uwekezaji huo usiwe wa kiwango kinachoweza kuunda dalili ya mzozo wa upendeleo..
Kuanza na mwisho ndicho kitu cha msingi katika biashara ya ushirikiano. Hii hujibu swali; hivi mimi na mshirika wangu wa kibiashara tunamalengo sawa? Tunajisoma? Tunajifunza mambo mapya kilasiku? Tunasoma vitabu vya utambuzi na maarifa ya biashara? Mshirika wangu na mawazo hasi ama chanya?
Anamvuto? Ana dira ya maisha?  Ana aminini katika misemo ya ponda mali kufa kwaja? Maisha yake ameyaweke rehani kwa wanasiasa? Au ana amini kwamba mkombozi wake ni serikali au kiongozi wake wa kisiasa? Mkijua kila mmoja ana lengo na nini na kwanini?,kwa vipi?  ni muhimu kuliko kufanya mambo kienyeji ambayo huleta faida za kienyeji na mwisho wa kienyeji. Kwaleo niishie hapa. Sisi sote ni washindi-na tunahitaji ushirikiano.




















Meshack Maganga---Go Big Or Go Home
Previous
Next Post »