.

Mafumbo Makubwa Mawili Kwenye Mafanikio...!

  Na: Mrope Wa Mrope- Iringa

HAKUNA MASHINDANO MAZURI KAMA MASHINDANO YA KUSAKA MAFANIKIO YAKO MAANA YENYEWE YAPO KILA SIKU KATIKA KUISHI KWAKO (HAYASUBIRI MSIMU).
Katika uhai wa binadamu kuna mafumbo makubwa mawili; 1. Kwanini nililizaliwa? (kusudi la kuja duniani) 2. Lini nitaondoka duniani? (hicho kilichonifanya nizaliwe kitakuwa kimetimia?). Kwa hiyo haya mambo mawili ndiyo yanayotawala maisha ya mtu yeyote. Akiyajua ni heri kwake lakini asipoyajua ni
majuto kwake.
Nakumbuka nikiwa mdogo kabisa nilikuwa sielewi kwanini nipo duniani? Nilikuwa nauangalia mwili wangu na kujiuliza, "huu ndio wanauita Aloyce?" tena mara nyingi nilikuwa nafanya hivyo huku naufinya mwili wangu (nilikuwa sioni thamani yake? Sina hakika). Nilikuwa najiuliza, "hivi siku nikifa huu mwili unaoitwa Aloyce wataufikia na wakiufikia nini hatma ya huu mwili unaoitwa Aloyce?".
Nakumbuka vyema kuwa sikuwa na raha na hali hiyo ilidumu kichwani mwangu kwa miaka mingi ya utoto mpaka nilipoanza darasa la kwanza nikiwa nina miaka 10.
Kabla ya hapo nilikuwa nasahau ninapokuwa katika michezo mbalimbali na nafikiri nilipoanza shule ile hali ilikwsha kwa kuwa nilikuwa bize shule na nikitoka bize kwenda kucheza.
Sasa nimekuwa ninaelewa kwa yakini kuwa kama huna malengo yanayokupa changamoto na himizo la kutenda mambo fulani unaweza usione sababu ya kuishi na unaweza kupoteza kabisa matumaini ya kuishi. Mwaka huu mtu mmoja aliniuliza tena akiwa hana matumaini ya kupata jibu la hakika, "wewe si mbeba maono? Niambie kwanini tunaishi maana mimi naona tunatafuta pesa tunakula, tunavaa na kulala basi, sasa hiyo tu ndiyo sababu ya kuishi?". Nilimjibu kwa kifupi, "Tumezaliwa ili kuleta mabadiliko huko kula, kuvaa na kulala ni mambo ya msingi ili tuweze kuishi tunapoleta mabadiliko".
Wakati mwingine mtu kama anaishi kwa kutazama mkate tu, sio tu atakufa maskini bali pia atapoteza matumaini ya kuishi na atafikiri hapa duniani ni stendi ya kusubiria kifo. Kama dunia ingekuwa stendi ya kusubiri kifo basi tusingezaliwa tungebaki huko huko bila "kusumbuliwa" roho zetu.
Bahati mbaya wimbi kubwa sana la watu linafikiria kusubiri kufa ndio maana wana misemo yao, "ponda mali kufa kwaja" lakini hawapondi mali bali wanaponda kidogo walichonacho na kufa hawafi ila cha moto wanakiona. Kumbe ili mtu adumu katika furaha na amani ni vyema akatambua anatakiwa kuleta mabadiliko maana itamsaidia kuishi kwa malengo na nidhamu katika nyakati zake zote za kuwa chini ya jua. Hakuna mtu mwenye dhamira ya kuleta mabadiliko chini ya jua "akaponda mali".
Hakuna mtu aliyedhamiria kuleta mabadiliko chini ya jua akafanyia jambo jema jamii yake akajivuna au kuwadharau watu wale, "kama si mimi kujenga shule yangu kule basi wangebaki wajinga mpaka mwisho wa dunia", hawezi kujitapa maana anatimiza malengo yake ya kuwa hapa duniani na wala hamsaidii mwingine.
Kwa kutojua haya tumejenga jamii ya watu wenye kiburi, dharau na majivuno maana hata wanapoleta mabadiliko ambayo ni wajibu wao wa kuwa duniani wanadharau na kutukana wengine. Kila mmoja wetu ana deni lake na anapaswa kulilipa na kama asipolipa kwa jeuri zake mimi sijui nini kitatokea.
Nakumbuka nilipojiuliza thamani yangu niligundua sina thamani na nikaamua kuongeza thamani yangu kwa kutafuta ushindi katika michezo, darasani na hata katika kuzungumza.
Nilikuwa nikijisemea, "mwili hata utakapofukiwa utakuwa na thamani" (katika mawazo ya utoto). Kwanini nimetimiza makusudi ya kuzaliwa kwangu? La hasha hata robo bado ila nami najitutumua kufanya kusudi la kuzaliwa kwangu ili hata katika kufa kwangu ikiwa nitakuwa sijatimiza nitakuwa nilikuwa nipo katika barabara ya kutimiza.
Kwa hiyo jambo la kwanza mtu ajue kusudi la kuzaliwa ni kuleta mabadiliko, mabadiliko katika eneo lipi? Hapo hatuwezi kufanana. Ukijua kusudi la uwepo wako utapambana daima ili utimize na yale mapambano ya kupata na kukosa yatakupa burudani ya kuishi.
ALOYCE MROPE, Che Mrope wa Mrope (fb) Mbeba Maono (fb page) 0766656626/0787641417/0715366010
Previous
Next Post »