Na : Albert Sanga- Iringa
Mwaka 2008 nilifunguo chuo cha
mafunzo ya kompyuta(Stepwise Universal College) huko wilayani Mufindi
Iringa. Mbali na mafunzo ya kompyuta na ukatibu mahsusi(Secretarial
Courses), chuo kilikuwa kikifanya biashara ya kutoa huduma ya
Internet(kwa mtandao wa TTCL).
Wakati huo simu za mkononi zenye internet
zilikuwa chache na gharama sana; hivyo; wateja hawakuwa na chaguo
katika maeneo yale zaidi ya "kuniungisha"; ambapo lisaa limoja tulikuwa
tunachaji Tsh. 5,000 (elfu tano hii
unayoijua) na asikwambie mtu nilikuwa natengeneza hela kama "mvua" na
faida ilikuwa kubwa kupindukia(supernormal profit). Mwaka 2010
nikajaribu kufungua tawi mjini Makambako, nikitegemea mambo yatakwenda
kama nilikoanzia; looh! Nilipofika hapo kwanza nikakuta kuna "internet
cafes" nyingi pili wakawa wanachaji Tsh. 1,000 tu kwa lisaa! Faida
ikapungua mara tano! Si hivo tu, punde si punde, simu za mchina zikaanza
kuingia kwa fujo kiasi kwamba kupata wateja ikawa ni mara moja moja
sana.
Mwaka 2011 nikajaribu kuhamishia biashara hizi Iringa mjini, ila
nikagundua ni kugumu mara mia ya nilikoanzia. Baadae niliuza ile
biashara yote nikaingia kwenye biashara zingine. Nimekusimulia hii ili
nipate upenyo wa kukueleza mambo matatu kuhusu biashara. 1) Biashara
zinabadilika kwa spidi sana, kuzalisha faida kwenye biashara (hasa
nyakati hizi) unahitaji timing ya hali ya juu sana.
Watu wamekuwa
wajanja sana, wanaiga haraka na wanatafiti sana. Leo "ukiotea" biashara
inayokupa faida kubwa, watu wanakupa miezi michache, wanakusoma halafu
ghafla bin vuu utaona kila mtu kaanzisha biashara kama yako; usipokuwa
mjanja wa kubadilika ama kuboresha; mtaanza kunyang'anyana wateja na
utajikuta biashara inakuwea ngumu na hata kufa. Kilichonipata mimi ni
kuwa biashara ya internet ilikuwa inabadilika halafu mimi nilibakia na
mawazo ya kizamani, kutegemea faida kubwa bila ubunifu mpya!
Usinicheke!! Nenda kawaulize wafanyabiashara waliotikisa kwa biashara ya
vibanda vya kupigisha simu, halafu wakawa wazito wa kusoma upepo na
kubadilika! 2) Unapotaka kuanzisha biashara hakikisha una taarifa
halisi na za karibuni kuhusu biashara hiyo, vinginevyo utaliwa.
Kwa kuwa
ulisikia mwaka jana kuwa bodaboda zinalipa, unakimbilia leo kuchukua
mkopo na kununua bodaboda kumbe hiyo biashara imeshaingiliwa na mdudu!
Kwa kuwa huko nyuma ulisikia biashara ya nazi inalipa, unajichomeka
kuingiza mtaji, kumbe huna habari kuwa Azam siku hizi anasindika nazi na
kuuza kwenye pakiti; nazi zako zitadoda! 3) MWISHO NINAKUPA RAI: Karibu
kwenye ulimwengu wa biashara na ujasiriamali; ila jiandae kiakili, huku
hakuna "hit and win", kuna hitaji misuli, uvumilivu, ujanja na moyo wa
chuma; uzuri ni kuwa "anaejaribu" tena na tena bila kukata tamaa ndie
"ANAE-WIN" ~SmartMind~
Sign up here with your email