.

Wajasiriamali Wengi Hudhani kuwa Mteja Ndie Mwenye Shida...!

Na:  Albert Sanga, Iringa.

Siku moja nilikuwa mjini Mafinga wilayani Mufindi katika mkoa wa Iringa. Nikiwa hapo nikaingia kwenye duka moja la vifaa vya ujenzi nikiwa na lengo la kununu a vifaa kadhaa vyenye thamani ya takribani shilingi laki tatu. Katika duka hilo nikamkuta mama mmoja ambaye wakati akinipokea alionekana kuwa bize kubonyeza simu yake ya kiganjani. Nilipomsalimia hakujibu  na baada ya (SOMA ZAIDI)
kuinuka kutoka katika kuitazama simu yake akaniuliza, “Nikusaidie nini?” Mimi nikamjibu kwa kumueleza vifaa ninavyovihitaji  na kumuomba anitajie bei zake kimoja kimoja. 

Kwa haraka haraka akanitajia bei ya vitu vyote na ndipo nikamuuliza swali jingine “Utanipunguzia kiasi gani?” Akajibu  kimkato, “Sipunguzi”. Wakati akinipatia jibu hilo tayari simu yake ya kiganjani alishakuwa ameiweka masikinoni mwake akiongea kwa kucheka na kufurahi kweli kweli.
Pamoja na kunipatia jibu hilo la kuwa hapunguzi chochote bado nikamweleza kuwa ninaomba anipatie bidhaa nilizozihitaji. Kwa kuwa alishakuwa bize na kuongea kwenye simu alinipuuza nami  nikaendelea kusubiri kwa dakika zaidi ya tano. Nilipoona kuwa hashtuki wala hanijali nikalazimika kuondoka dukani hapo na kwenda duka jingine. 

Licha ya kuanza kuondoka huku  nikiwa na shilingi laki tatu mkononi lakini bado mama Yule hakuonesha dalili yeyote ya kukata simu ili anihudumie. Kilichonisikitisha ni kuwa kilichokuwa kikiongelewa kwenye simu yalikuwa ni mambo ya mmisuko ya nywele na mishono ya vitenge!
Siku nyingine tena nilikuwa Iringa mjini mtaa wa Uhindini na nikafika katika duka la mswahili mmoja ambaye anajishughulisha na uchapaji wa tshirts. Nilipofika nilikuta amenuna sana na nilipomsalimia hakunijibu. Nakaona isiwe tabu kutojibiwa salamu, wacha nishughulike na lililonileta ambalo lilikuwa ni kuuliza bei za kuchapishiwa tshirts. 

Nilipomuuliza maswali matatu ambayo kimsingi ilikuwa ni kutaka kupata maelezo ya kina, nikakuta ghafla amekasirika na akaanza kunifokea, “Wewe mteja msumbufu sana, kama unataka tshirts sema tukuchapishie lakini kuulizwa maswali mara mbili mbili mimi sitaki. Au kama vipi katafute kwingine mimi kwangu sitaki!” 

Jibu hili lilifanya nipigwe na butwaa kwa sekunde kadhaa nikiwa siamini ninayosikia.  Nikatoka pale na nikatafuta na kupata eneo jingine ambako kuna Wahindi ambao wanafanya pia shughuli za uchapishaji. Nilipoingia tu ofisini kwa hawa Wahindi nikakaribishwa kwa bashasha kubwa na kuelekezwa kiti cha kukaa. 

Punde nikaletewa soda halafu  nikaulizwa, “Tukusaidie nini mheshimiwa?” Huhitaji kuwa mtabiri kuelewa ni nini kilifuatia kwa sababu waliongea nami kwa ukarimu, ucheshi na bashasha nyingi kiasi kwamba nikajikuta nimewapa tenda ile pale pale.
Tuko katika zama ambazo mteja sio tu kwamba ni mfalme, isipokuwa mteja ndie serikali kamili katika biashara yako. Mteja anaweza kukupatia faida lakini anaweza kukupatia hasara. Zama hizi zina ushindani mkubwa kiasi kwamba bidhaa ama huduma za aina moja zinapatikana kwa wauzaji zaidi ya mmoja na kwa bei za kiushindani. Mteja hafungwi bali anaamua kuhudumiwa ama kununua popote. Hizi ni zama ambazo zinatawaliwa na huduma kwa wateja yaani kuwajali, kuwasikiliza na kuwafanya ni sehemu ya familia.

Yapo mambo kadhaa yaliyopelekea suala la kumjali mteja kuwa ni kipaumbele cha kwanza katika zama hizi za kibiashara. La kwanza linatokana na ushindani na usawa wa kimasoko ambapo watoa huduma, wazalishaji  pamoja na mamlaka wanadhibiti na kuamua bei sokoni. 

Mathalani wazalishaji wa soda wanapopeleka soda zao kwa wauzaji wa rejareja wanawapangia na bei kabisa, mfano shilingi 600/=. Hii ina maana kama wewe una duka na umeweka soda, halafu na duka la jirani yako nae ana soda; moja kwa moja ni kuwa bei yenu ya kuuzia soda itakuwa ni ile ile yaani shilingi 600/=. 

Kama wewe unauza bei hiyo hiyo anayouza jirani yako, unadhani ni nini kitamsababisha mteja aache kununua kwa jirani yako aje kununua kwako? Jibu ni kuwa (pamoja na viambata vingine) kitu atakachozingatia mteja ni namna biashara husika inavyomjali na kumthamini.

Jambo la pili linalofanya huduma kwa wateja iwe na kipaumbele zama za sasa ni namna utamaduni wa jamii zetu unavyobadilika. Tumekuwa na jamii iliyokosa upendo, jamii yenye migogoro ya aina nyingi, jamii isiyothamini utu wa wanadamu pamoja na jamii isiyojali hisia za watu wengine. 

Kutokana na haya watu wanatafuta faraja, wanatafuta kuthaminiwa, wanatafuta kuheshimiwa. Mahali popote ambapo mtu aliyekosa faraja, upendo na heshima atahisi anapata vitu hivyo atapakimbilia. Mteja atashikika katika biashara yako atakapogundua kuwa anapofika dukani kwako kununua soda anapata na faraja, anapata na heshima na anapata na ukarimu kwa namna muuzaji anavyompokea, kumsikiliza na kumuhudumia. 

Mteja anapofika dukani kwako kununua nguo anahitaji zaidi ya nguo. Ikitokea unamsifu namna alivyopendeza, unamuhakikishia kuwa kwa nguo hiyo atakubalika zaidi na zaidi; inampa faraja, tumaini na kujisikia vizuri mteja huyu. 

Kwa nyakati hizi ili uweze kuwa na wateja wengi na wanaodumu ni lazima mjasiriamali ujifunze namna ya kuambatanisha huduma ambazo zinaziba pengo la mambo niliyoyataja ambayo jamii inayapuuza ama inajimomonyoa kuyazingatia.

Jambo la tatu ni kukua kwa teknolojia ya mawasiliano. Changamoto hii nimekuwa nikiirudiarudia ili wajasiriamali tujifunze hatari iliyopo mbele na tuchukue hadhari. Uwepo wa mawasiliano yaliyoimarika yanafanya wateja wengi kufahamu ni nini kinafanyika huko kwa wenzetu.
Sote tunafahamu kuwa huko nje kwa wenzetu walioendelea, huduma kwa wateja ipo juu sana. Kwa urahisi wa mawasiliano mteja anaweza kuachana na kununua bidhaa kutoka duka la pale Kariakoo na akaamua kununua kutoka Tokyo Japan!

Wajasiriamali wengi wanashindwa namna ya kuwajali wateja halafu wanaishia kusema biashara siku hizi ni ngumu. Biashara itakuwaje nzuri wakati mtu akiingia dukani kwako anahisi kama ameingia kuzimu kwenye mateso? Biashara itakuwaje nzuri wakati mteja akifika biasharani kwako anaondoka akiwa na msongo wa mawazo?

Kitu ambacho mjasiriamali unatakiwa kufahamu ni kuwa kuanzisha biashara pekee hakutoshi kukuhakikishia mafanikio. Kufungua mlango wa duka na kupanga bidhaa hakukupi garantii yaw ewe kupata wateja. Wateja wote wanapenda wanapoingia katika biashara yako wajisikie wapo zaidi ya nyumbani. 

Lakini wakati wote unapokuwa na biashara jitahidi kuwa na vitu vilivyokamilika. Huwa nashangaa sana ninapokwenda dukani kununua kitu nikiwa na noti kubwa halafu muuzaji ananiambia sina chenji. Huwa najiuliza, jukumu la kutafuta chenji ni langu mimi mteja ama la muuzaji?
Kama chenji hamna basi ni vema ukaandika dukani kwako “hatupokei noti kubwa kwa sababu chenji hatuna!”. Sasa fikiria biashara imeshinda asubuhi hadi jioni inatoa majibu ya chenji hamna halafu jioni mjasiriamali anasema “leo biashara imekuwa ngumu!”. Wajasiriamali tunahitaji umakini katika eneo hili mambo madogo madogo katika biashara zetu ndiyo yanayotuangusha

Wajasiriamali wengi hudhani kuwa mteja ndie mwenye shinda, lakini kimsingi mwenye shida ni wewe uliyeanzisha biashara ili upate faida. Wale waleta faida ambao ndio wateja unatakiwa uwanyenyekee na kuwathamini sana, vinginevyo shida yako ya kupata faida haiwezi kutatulika.
Ni vema kuwa makini sana katika suala la kuajiri wafanyakazi wanaoshinda kwenye biashara zetu, kwenye ofisi zetu na kwenye maduka yetu. Wale wanaofuatilia makala zangu wanakumbuka makala mbili nilizopata kuandika huko nyuma: 

Ya kwanza, “Mjasiriamali na Sayansi ya kuajiri wafanyakazi” na Ya pili ilikuwa na Kichwa, “Wafanyakazi wazembe ni mzigo kwa Wajasiriamali”. Katika makala hizo nilisisitiza wajasiriamali kuwa na umakini mkubwa katika kutafuta, kuajiri na kuishi na wafanyakazi.

Hata katika suala hili la kuwajali wateja, utafiti unaonesha kuwa wajasiriamali wenyewe (yaani wamiliki wa biashara husika) huwa wananidhamu sana katika kuwajali wateja. Huwa hawana makuu, hawana dharau wala maringo kwa wateja. Pengine ni kwa sababu wanafahamu uchungu wa biashara zao na malengo yao ya kuzalisha faida. 

Tatizo kubwa huwa ni kwa hawa wafanyakazi wanaoajiriwa. Wengi wao hawajabeba mioyoni mwao maono ya biashara wanazofanyia kazi. Wengi wao huwa hawafanyi kwa moyo biashara hizo na ndio chanzo cha kudharau wateja, kuwabeza na kuwapuuza wateja.

Shida ni kwamba mfanyakazi anaposhindwa kumjali mteja anaeumia ni mjasiriamali anaemiliki biashara husika. Mteja akimchukia muuzaji ama mfanyakazi uhalisia ni kwamba atakuwa ameichukia na biashara yenyewe. 

Kwenye biashara kuna msemo usemao ni rahisi kumpata mteja mpya katika biashara kuliko kumrejsha mteja aliyepotea. Biashara yako inaposhindwa kuzingatia huduma bora kwa wateja ni rahisi mno kupoteza wateja.

Nihitimishe kwa kusema kuwa pengine ule msemo wa mteja ni mfalme kwa sasa umeisha kabisa kabisa. Tulichonacho kwa zama za sasa ni hiki, ‘Mteja ni sehemu ya familia”. Mteja anatakiwa kutendewa kwa ukarimu, anatakiwa kusaidiwa hata baada ya kununua ama kuhudumiwa, anatakiwa kuthaminiwa hisia zake. Wajasiriamali watakaofanikiwa nyakati tunazoziendea ni wale watakaowekeza ubunifu katika kuziteka saikolojia, hisia, mitazamo na mitindo ya kimasha ya wateja wao; ambavyo vyote vimo katika hiki kiitwacho kumjali mteja.
stepwiseexpert@gmail.com +255 719 127 901
Previous
Next Post »