Na: Albert Sanga,
Iringa.
Hivi karibuni kulikuwa
na habari iliyotikisa vyombo vya habari hasa kwenye mitandao ya kijamii
iliyohusu usaili wa idara ya uhamiaji. Idara hiyo ilitangaza nafasi zisizozidi
sabini lakini walioitwa kwenye usaili walikuwa waombaji zaidi ya elfu kumi
(10,000). Usaili ule ulifanyika kwenye uwanja wa taifa kiasi kwamba ukitazama
zile picha ungedhani lilikuwa ni rundo la watazamaji wa mpira wa miguu.
Tukio lile lilizua
hisia tofauti miongoni mwa wengi, wengi wakimwaga lawama kwa serikali na
kuonesha hofu yao kuhusu tunakoelekea na hili tatizo la ukosefu wa ajira.
Binafsi nilipoliona tukio lile nililitazama kwa jicho jingine na nilifurahi,
kuona tumefika mahala pazuri kama utakavyoona kwa kadiri ninavyoendelea
kuchambua hapa.
Kwanza ifahamike kwamba
tatizo la ukosefu wa ajira lipo dunia nzima. Hata zile nchi zinazotufadhili
tatizo hili linawatafuna kule kwao. Mathalani ukosefu wa ajira nchini Marekani
ni asilimia 6.1% na Uingereza ni asilimia 6.8%, ilhali Tanzania ni asilimia
11.7%. Kwa hiyo tunapolitazama tatizo hili tuhakikishe tunalipatia sura ya
kidunia kitu kitakachotusaidia kufikiria na kupata majibu halisi kwa mujibu wa
hali inayoendelea ulimwenguni pote.
Katika nchi nyingi
zilizoendelea na hata katika mataifa mbalimbali yanayoendelea Afrika ikiwemo
Misri, Nigeria, Tunisia na nyingine; ukosefu wa ajira ndio ulioboresha
ujasiriamali. Baada ya kuona ajira hakuna, baada ya kuona serikali imeelemewa,
wananchi wengi katika mataifa hayo walianza kuumiza vichwa namna ya kujikwamua
kama mtu mmoja mmoja. Ndipo ubunifu wa biashara, kuona fursa ndogo na kubwa
kulipoendelea kuwa sehemu ya utamaduni na maisha ya kila siku kiuchumi.
Kinachowafanya vijana
wengi katika nchi yetu Tanzania, kutoona namna ya kujiajiri ni kwamba bado
shida hazijawapiga ipasavyo na kama zimewapiga ipasavyo basi bado
hawajazinduka. Wengi wa vijana wetu wanapomaliza masomo yao bado
hawajafikia
hatua ya kukosa chakula, kukosa pa kulala na pengine kukosa mavazi.
Hata wakiwa hawana ajira
wanakula, wanapo pa kulala na wanavaa vizuri. Wanamudu haya kwa sababu jamii na
familia zetu nyingi bado tuna utamaduni wa kijamaa. Kijana anahitimu masomo
yake leo lakini anaweza kuishi kwa mjomba, kaka, dada, mzazi, binamu, mtu wa
kutoka eneo moja; hata kwa mwaka mzima akila, akilala na akivaa eidha kwa
kisingizio cha kutafuta ajira ama kwa kigezo cha “kwa sababu hana ajira”.
Huu mtindo unachangia
sana kudumaza akili za ubunifu kwa vijana wetu wasomi, hawaoni fursa kwa sababu
hakuna kitu kinachowalazimisha kuziona. Shida, matatizo na changamoto ni kani
(nguvu) zenye mchango mkubwa kumsukuma mtu kuziona fursa.Kwa kadiri shida,
matatizo na changamoto zinavyozidi kuwa kubwa ndivyo ambavyo uwezekano wa mtu
kuona fursa ndogo ndogo unavyozidi kuongezeka. Kama hujabanwa vizuri na
matatizo ni rahisi kudharau fursa fulani fulani.
Hebu tujiulize hadi
sasa ni vijana wangapi wanahitimu vyuo vikuu na kuthubutu kwenda kutafuta
vibarua vya kukata majani ya mifugo kwa wafugaji? Ni wasomi wangapi baada ya
kukosa ajira wamediriki kuanza biashara ya kutembeza maji mitaani, kwenye
stendi na sehemu zenye watu?
Tunao vijana wangapi
wahitimu wa shahada, stashahada na vyeti wenye nguvu na afya zao ambao baada ya
kukosa ajira wameamua kukaa kwenye masoko mbalimbali kufanya tenda za kushusha
mizigo? Niambie tuna vijana asilimia ngapi ambao wanauthubutu wa kuweka tai zao
chini na kuamua kuwafuata wenye maduka ili wawe vibarua wa kusogeza mizigo
stoo? Kilimo kinalipa, lakini ni vijana wangapi wenye shahada zao ambao
wanaweza kuweka vyeti vyao kwenye makabati kisha wakapiga kambi vijijini huko
mashambani kwa ajili ya kulima?
Kimsingi vijana
hawawezi kuona kuwa kukata majani ni fursa hata kama wana digrii kwa sababu
bado shida hazijawapiga vizuri. Hawawezi kuona kana kwamba kutembeza maji
mtaani ni fursa kwa sababu wanapo pa kulala, wanapo pa kula, wanazo simu za
gharama zinazowafariji kwa mitandao ya kijamii na bado wanavaa vizuri.
Nakuthibitishia kuwa kijana
iwe ana shahada ya uzamili, shahada, stashahada ama cheti, ikitokea mambo
yamemuwea magumu kabisa; hana pa kulala, hana pa kula hana mavazi ya kuvaa;
hawezi kukataa kazi ya kufyeka majani, hawezi kudharau kazi ya kulima, hawezi
kujivunga kwenda kushusha mizigo stendi wala hawezi kudharau fursa yeyote hata
kama itamletea shilingi hamsini. Atathubutu, atatenda na atafanikiwa!
Ukienda kule Nigeria ni
kawaida kukuta vijana wenye shahada za uzamili na shahada wakipiga rangi za
viatu mitaani, wakiuza maji na wakizunguka na bidhaa kiumachinga. Hata kule
Misri kilichoibua hasira za maandamano yaliyoung’oa utawala wa Rais Husein
Mbarak ilikuwa ni baada ya askari wa jiji kumnyanyasa kijana msomi wa chuo
kikuu ambae aliamua kujiajiri kwa kuanzisha banda la ‘umachinga’ baada ya
kukosa ajira.
Vijana wasomi kuwa
machinga, wapiga debe, wabeba mizigo, wakata majani na wakulima wadogo wadogo;
mtu anaweza kusema ni ‘bomu’. Lakini ukweli ni kwamba hiyo ni nukta nzuri.
Wasio na ajira (wawe wasomi ama wasiosoma) wanapopatwa changamoto kiuchumi
kisha wakawa tayari kuzichangamkia fursa ndogo ndogo na zinazodharauliwa, hiyo
ni hatua nzuri sana.
Mara nyingi nimekuwa
nikisema na kurudia kuwa tatizo la Tanzania sio ukosefu wa ajira bali kuna
umasikini mkubwa wa kifikra unaosababisha watu kutouona uwezo wao wa ndani na
kushindwa kuona fursa zinazowazunguka. Hapa ndipo tunapotakiwa kuwekeza sio
kumwaga misaada na mikopo ya fedha pekee.
Ongea na vijana(wasomi
na wasiosoma), kina mama, na wengine kuhusu kujikwamua kiuchumi; kilio chao
watakueleza ni ukosefu wa ajira na kuhusu kujiajiri watakutolea machozi kwamba
wanakosa mitaji (fedha). Sasa jaribu kuwachukua vijana wasomi waulize huu
ukosefu wa fedha ni kiasi gani kinahitajika katika biashara zipi?Wengi utaona
wanakutajia biashara kubwa kubwa za mamilioni ya fedha.
Kitu ninachosema na
kusisitiza ni kuwa tatizo la ukosefu wa ajira litaendelea kuwa kubwa mpaka pale
wahusika watakapoweza kuwa na ufahamu wa “kiupambanaji” ambao unaiona shilingi
elfu moja kama mtaji mkubwa. Bahati mbaya ni kuwa tuna kizazi cha wasomi (na
watanzania wengi) ambao utafutaji wa maarifa sio kipaumbele kwao.
Lakini katika kitabu
changu, kwenye chambuzi zangu na kwenye semina zangu nimekuwa nikieleza kwa
mifano namna unavyoweza kuzalisha fedha pasipo fedha. Hivyo utabaini kuwa
sababu nyingine ya vijana wetu wasomi na Watanzania kwa ujumla kulalamika kuwa
wanashindwa kujiajiri kwa kukosa fedha (mtaji) ni kwa sababu hawana maarifa ya
namna ya kuzalisha fedha pasipo fedha. Maandiko matakatifu yanaonya kuwa “Watu
wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”
Wasomi wetu wana maneno
mengi ya kujitetea na kulalamika kwa sababu bado wanaishi kwa falsafa za kale
katika zama mpya. Enzi hizo ilikuwa “soma upate kazi” lakini siku hizi ni “soma
utengeneze kazi”. Kwa zamani nchi yetu ilikuwa chini kielimu, waliokuwa
wakisoma walikuwa wachachena wote ilibidi kupata kazi kutokana na mahitaji.
Siku hizi mwamko wa
elimu umekuwa mkubwa, shule na vyuo vinaongezeka kila siku, kwa hiyo ndoto za
“soma upate kazi” inazidi kuyeyuka. Msomi yeyote ambaye anasoma kwa mtazamo wa “soma upate kazi” ni rahisi
sana kuchanganyikiwa anapoingia mtaani na kukuta kazi hamna.
Kwa hiyo, tatizo hili
la ajira linavyozidi kuongezeka, tunavyozidi kuwa na vijana wengi wasomi wasio
na kazi mtaani, ndivyo maisha yatakavyozidi kuwa magumu zaidi na zaidi. Huu
mtindo wa kijamaa wa kula, kulala na kuvaa kwa mjomba, kaka, binamu; unazidi
kuisha kutokana na ugumu wa maisha.
Maisha yanapozidi kuwa magumu
kwa waliokosa ajira, wajomba wanapoendelea kuchoka kulisha na kulaza wasio na
ajira; itakuja nukta ambayo aliekosa ajira hatakuwa na namna isipokuwa kuziona
fursa hata zile fursa ndogo ndogo zinazodharauliwa ziwezazo kumuokoa kiuchumi.
Hapo ndipo ninaposema tumefika pazuri, kwa sababu akili zitakuja.
Hili wimbi la ukosefu
wa ajira halina haja ya kulihofia kwa sababu hizi akili za watanzania wengi
haziwezi kubadilika tusipopitia tunapopita sasa. Vijana wetu wamekuwa wavivu wa
kubuni, hawana maono kuhusu kesho zao, wamekuwa mabingwa wa kuchagua kazi, wana
ndoto za maisha makubwa ya kulala masikini na kuamka matajiri, hawana utamaduni
imara wa kujifunza na kujisomea kuyajua maisha halisi kutwa kucha wanahangaika
kuota maisha ya ‘mamtoni’, maisha ya kwenye filamu na maigizo. Akili kama hizi
sio rahisi sana kubadilika mpaka shida ziwachakaze kisawasawa, hapo ndipo
watazinduka.
Kwenye kitabu changu cha “Ni wakati wako wa Kung’aa” katika
sura inayoeleza namna mtu unavyoweza kuzalisha fedha pasipo kutumia fedha,
nimeeleza nguvu mbili ziitwazo “Push power” na “Pull Power” zinav yowasukuma watu kutafuta mafanikio. Nimeeleza kuwa unapokuwa
katika matatizo makubwa halafu kukawa hakuna namna unayoweza kutulia ama kurudi
nyuma, hapo unatakiwa kutumia “push power”.
Hii ni nguvu ambayo
inaambatana na mtu pale anapobaini kuwa akitulia na kulia-lia matatizo
yatammaliza; hivyo anaamua kupambana. Na anapokuwa akipambana huku akijua kuwa
alikotoka ni kubaya na hakufai kurudi, basi hataacha kupambana zaidi na zaidi.Wakati
utakuja ambapo mtu aliekosa ajira yeye mwenyewe atainuka kwenda kuchakarika
pasipo kuililia serikali.
Kuna mazingira ambayo
serikali imekwisha yaandaa yanayoweza kuwasaidia watu kujiajiri lakini
hayajatumika kwa asilimia 100%. Kabla ya kuilalamikia na kuililia serikali hebu
yatumike kwa asilimia 100%. Lakini hili tatizo la ukosefu wa ajira tupende ama
tusipende litatuletea akili za kujitegemea na kupambana.
Inawezekana kila
Mtanzania kuwa mshindi wa kiuchumi!
0719
127 901 stepwiseexpert@gmail.com
Sign up here with your email