Na: Albert Sanga, Iringa
Wakati fulani nimewahi
kufanya biashara ya daladala na nilikuwa na magari kama matatu hivi.
wafuatiliajI wa safu hii
bila haka mnakumbuka kuwa wakati fulani huko nyuma nimewahi kuchambua kwa kina
chungu na tamu za biashara za daladala. Si kuudi langu leo kuelezea ‘chungu na
tamu’ za biashara za daladala, isipokuwa kuna
uzoefu nataka niutohoe kutoka
kwenye biashara hii kuhusu wafanyakazi.
Kwa kumiliki magari
matatu niliweza kuajiri wafanyakazi saba; madereva watatu, makondakta watatu na
msimamizi mmoja. Kuna mambo yanapelekesha katika biashara ya daladala, mojawapo
kubwa likiwa ni wafanyakazi. Ngoja nikupe visa viwili vinavyowahusu.
Kwa kawaida niliweka
utaratibu kwamba magari yote ni lazima yawe yamepaki kabla ya saa mbili usiku
na mahesabu ya siku yawe yamewasilishwa. Siku moja gari mojawapo likaonekana
halijapaki kwa muda husika na dereva wala kondakta wote hawapatikani kwenye
simu. Usiku ukapita, kesho ikafika gari halijaonekana wala dereva hajulikani
alipo.
Msako na upelelezi
vikaanza na hatimaye nikapata taarifa kuwa gari ilikodiwa kwenda kijiji fulani
umbali wa kilomita themanini kutoka Iringa mjini. Kutokana na ubovu wa barabara
gari ikaharibu difu na kutoboa ‘sample(kifaa kinachotunza oili)’. Baada ya
‘sample’ kutoboka hawakutilia manani, wakaendelea kutembeza gari na hatimaye
ikaua injini. Nikatoka na gari nyingine tukaenda kuivuta na baada ya hapo
nikawafukuza kazi dereva na kondakta wake.
Kisa cha pili; siku moja
majira ya saa tatu usiku nikapigiwa simu, “Hallo, wewe ndie Nyaluke? (jina la
biashara kwenye magari nilikuwa nikitumia Nyaluke Trans)” Baada ya kujibu
akanipa taarifa, “Gari lako lipo hapa limegonga mtu na kisha limegonga nyumba
ya watu hivyo fika haraka”. Nikatoka mbio mbio kwenda eneo la tukio na
nikajionea ajali ambayo ilikuwa kama sinema vile.
Kumbe dereva baada ya
kukabidhi hesabu akachukua gari na kudai anakwenda kuliosha, badala yake
akaingia kunywa pombe. Akiwa amelewa, wakati anarudisha gari kwa kupaki
akagonga gari nyingine. Badala ya kusimama akaanza kukimbia na gari, katika
kukimbia akagonga mtu, na akaendelea kukimbia ndipo hatimaye akagonga nyumba na
yeye akakimbia. Huyu naye akaniachia hasara kubwa, gari likiwa limechakaa
nyang’anyang’a. Dereva alikutana na mkono wa sheria lakini hilo halikuweza
kufidia hasara kwa upande wangu.
Baadae nikaona hasara
zimezidi nikaamua kukata bima kubwa za magari yote; lakini hilo halikuwa
mwarobaini. Matatizo mengine yakaendelea kubaki ambayo kimsingi ndio
kichefuchefu kikubwa katika biashara ya daladala. Ugomvi na wafanyakazi ukawa
kwenye hesabu. Leo wanakuletea hesabu pungufu kisa biashara ilikuwa mbaya.
Kesho wakitaka kukuibia;
wanapiga ruti na wanapata hela za kuwatosha; kisha wanapeleka gari gereji,
‘wakizuga’ kuwa liliharibika! Na wakishaingia gereji ujue hesabu ya jioni
itakuwa ni hadithi. Acha hilo, kuna siku wanajisikia tu na hawaamshi gari,
achilia mbali makosa wanayofanya barabarani kiuzembe ambayo yanapelekea faini
za ‘kutosha’.
Fukuza fukuza ya
wafanyakazi, kuelimisha, kupangiana mikakati, kupelekana polisi; vyote hivyo
nilikuwa nikihangaika navyo, lakini mambo bado yalikuwa pasua kichwa. Kuna saa
nilikuwa nabahatika kupata madereva wazuri, lakini changamoto za wafanyakazi
‘vimeo’ zilizidi ‘unga’.
Baadae niliamua kuachana
na biashara hii na kuingia kwenye biashara zingine. Simaanishi kwamba biashara
ya daladala haina faida, la hasha! Faida ipo na mimi nilitengeneza faida kwa
kiasi chache. Ninachotaka ukione hapa ni kuwa ugumu ama changamoto katika
biashara hii unachangiwa pia na hulka waliyonayo wafanyakazi.
Ili uweze kuzalisha
biashara ya daladala inabidi uwe ‘ngumi mkononi’ yaani uwe mkali. Ukiwa wa
kucheka cheka na madereva na makonda, utavuna mabua, kwa maana utafika wakati
utajikuta gari limechakaa na fedha huna. Nini maana yake? Maana yake ni kwamba
kuna mushkeli upo kwenye mitazamo, tabia na uaminifu katikati ya wafanyakazi
walio wengi (sio wote) katika eneo hili.
Wafanyakazi vimeo katika
maeneo mbalimbali wamekuwa sababu ya biashara nyingi kufa, kupata hasara ama
hata kufungwa na wamiliki. Si hivyo tu lakini wapo watu wenye kiu ya kuanzisha
biashara lakini kila wakifikiria “nitapata wapi wafanyakazi waaminifu?”
wanaahirisha kufungua biashara zilizomo vichwani mwao.
Mathalani, kwa mimi
kupoteza magari mawili kwa uzembe wa wafanyakazi maana yake, ajira nne
zilipotea. Kwa kuamua kuachana kabisa na biashara hiyo maana yake kuna ajira
saba zilipotea. Je, ni watu wangapi ambao wanaamua kufunga ama kutoanzisha
kabisa biashara kutokana na tatizo la wafanyakazi waaminifu?
Mara nyingi kilio cha
ukosefu wa ajira kwa Tanzania tumekiweka kisiasa mno na tunakwepa uhalisia. Je,
ni watanzania wangapi ambao unapowapatia kazi hufanya kwa uaminifu na kwa
ufanisi? Ukitaka kufahamu hili, jaribu kuwatafuta wafanyabiashara wa maduka
(makubwa na madogo) watakueleza changamoto wanazopata kwa wafanyakazi wa kuuza
maduka.
Wamiliki wengi wa maduka
wanalia uhaba wa vijana waaminifu kwa ajili ya kuendesha(kuuza) maduka yao. Hii
ina maana wapo ambao huamua kufunga kabisa maduka yao, wapo ambao licha ya kuwa
wana mitaji lakini hawawezi kuanzisha maduka kutokana na ‘kukosekana kwa
wafanyakazi’. Vile vile wapo ambao wangeweza kufungua matawi ya biashara zao,
lakini wakifikiria “taabu” wanayopata kutoka kwa wafanyakazi waliopo wanakata
tamaa kabisa ya kufungua matawi mengine.
Kuna matatizo matatu
ambayo yanaliandama soko la ajira Tanzania. Mosi, ni uwezo wa watafuta ajira,
pili ni tabia za watafuta ajira na tatu ni maono ya watafuta ajira. Kuanzia
watafuta ajira wenye elimu kubwa, ya kati mpaka wale wasio na elimu kabisa.
Leo hii mtafuta ajira
anapotafuta ajira kichwani mwake anawaza kutajirika ndani ya muda mfupi. Vijana
wasomi leo wanapotafuta ajira wanafikiria ‘ghafla bin vuu’ wapate magari
‘makali’ wapate nyumba ‘zenye hadhi ya uhekalu’ na pia wawe na maisha kama ya
‘mamtoni’. Wenye elimu ndogo nao wana maono yao hatari kwa taasisi na biashara
wanazoajiriwa.
Tupo kwenye hali mbaya
kwa sababu hata ukimuajiri kijana wa kukutunzia ng’ombe nae anawaza ‘kutoka
kimaisha’ kwa kukuibia maziwa! Watafute wafugaji watakuambia namna wafanyakazi
walivyo pasua kichwa. Ukimuajiri muuza duka anaiba hadi mtaji kwa sababu nae
anataka awe na maisha mazuri ‘haraka haraka’. Haya ni maono hafifu na
yanatengeneza roho ya wizi kabla hata ajira haijapatikana
Uwezo wa kiutendaji nao
umekuwa ni tatizo kubwa. Nadhani hili limeanzia kwenye mifumo yetu ya kielimu
na utamaduni. Tumekuwa na mifumo ya elimu (kutoka chini mpaka vyuo vikuu)
ambayo inatia msisitizo katika nadharia na mitihani kuliko ujuzi na utendaji.
Si jambo la ajabu
kukutana na msomi, injinia, wa “Computer Software Production” ambaye hana uwezo
wa kutengeneza hizo “softawares” licha ya kwamba cheti kinaonesha kafaulu
vizuri. Mtu ambae ana vyeti lakini hana uwezo aajiriwe kwa lipi?
Lakini pia watanzania
wengi hatuna utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kwa kukimbizana. Wengi tuna
‘kauvivu’ fulani kuanzia katika shughuli zetu binafsi. Unamuajiri mtu kwa
mategemeo makubwa lakini unakuja kusikitishwa na ufanyaji kazi wake. Uvivu huu
umo katika kufikiri na kutenda ndio maana licha ya kwamba nchi hii imefurika
fursa, lakini wengi ‘wamezuia’ fikra zao zisione na hivyo wanaishia kuwa
“walalamishi”.
Wako wapi watanzania
ambao ukiwaajiri leo wanaweza kufanya kazi hizo kama za kwao? Katika ajira
nyingi za umma (hasa serikalini), hulka za wengi (wanaoajiriwa) ni kutochukulia
kwa umakini ajira zao. Lakini ni vema kufahamu kuwa sekta binafsi ndio
inayochukua hatamu za soko la ajira kwa sasa. Huwezi kuleta ‘ujanja ujanja’
katika sekta binafsi halafu ukategemea kubaki na ajira yako.
Hali ya soko la ajira,
tabia na mienendo ya wafanyakazi watarajiwa ilivyo inanifanya nijiridhishe
kwamba nchi hii haina tatizo la ajira, isipokuwa ina tatizo la “kutokuwepo na
wafanyakazi wa kutosha”. Hata katika sekta binafsi, kilio cha ukosefu wa mitaji
hakina mashiko (nimepata kulichambua hili mara nyingi); isipokuwa kuna ukosefu
wa maono, bidii, kujituma na fikra sahihi.
Badala ya kumwaga fedha
kwa tunaotaka wajiajiri, huu ni wakati mzuri wa kuwamwagia maono na kuwajengea
fikra. Ukimpa masikini fedha ujue unamuua, ila ukimpa maono huna sababu ya
kumpa fedha kwa sababu ataweza kujitafutia mtaji. Ikiwa “watafuta ajira”
watakuwa na maono, ninathibitisha pasipo shaka ya kwamba nchi hii ina ajira
nyingi kuliko idadi ya wananchi wote pamoja na watoto watakaozaliwa kesho!
Wiki iliyopita
nilibainisha kuwa nitaanza safari za mikoani kuzungumza na kubadilishana mawazo
na wafanyabiashara, wafanyakazi(kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi),
vikundi vya kiuchumi, wanavyuo, na watu binafsi; kwa lengo la kushirikishana
fursa, uzoefu wa biashara na mbinu zingine za kiuchumi.
Katika mialiko niliyopokea
kwa kwa awamu ya kwanza nitafika Lindi, Dodoma na Dar es Salaam. Ninashukuru
kwamba wapo ambao wameendelea kunialika. Ndugu mmoja kutoka Mwanza amenipa
mwaliko na nitazungumza katika semina ya kiuchumi inayoendelea kuandaliwa. Iwe
ni taasisi, kikundi ama mtu mmoja mmoja; ikiwa utatamani nifike/nipitie kwa
ajili ya maarifa ya kiuchumi na kibiashara, wasiliana nami mapema kwa ajili ya
kuingiza kwenye ratiba.
Kumbuka kuwa lengo kubwa
mwaka huu ni: “Kutengeneza wafanyabiashara wapya, na kuinua viwango vya wale
ambao tayari wapo katika biashara”. Hivyo ziara zangu mikoani ni sehemu ya
utekelezaji wa lengo hili ili kuipa maana na thamani zaidi safu hii. Unaweza
kuwasiliana nami moja kwa moja ama kupitia kwa Mratibu Mtendaji wa ziara hizi
Bw. Jonas, 0788 155010
Wasalaam!
0719
127 901, tepwiseexpert@gmail.com
Sign up here with your email